Rais wa Kenya William Ruto ameliambia taifa kuwa juhudi za mradi wake mpya wa kujenga makazi nchini unafanikiwa.
“Baada ya miaka miwili ya kazi ngumu chini ya mpango wa nyumba za bei nafuu, ninajivunia kutangaza uzinduzi wa uuzaji wa nyumba 4,888 unaokamilika sasa, katika miradi 21 ya makazi ya kijamii," alisema katika hotuba kwa taifa Alhamisi.
Nyumba hizi ni za vyumba kimoja kimoja, yenye vyumba viwili vya kulala na yenye vyumba vitatu vya kulala.
Amesema kuna vitengo 1,041 vya makazi ya kijamii, 2133 vitengo vya makazi vya bei nafuu na nyumba 1,714 za bei nafuu za watu wa tabaka la kati katika kaunti 24.
"Ninamwalika kila raia wa Kenya aliye na umri wa zaidi ya miaka 18 kujiunga na safari hii ya kihistoria kuelekea umiliki wa nyumba. Kwa kuongozwa na kanuni yetu ya haki - kitambulisho kimoja, nyumba moja, " Rais Ruto amesema.
Akitoa uhakikisho kuwa mchakato wa ugawaji utakuwa wa uwazi na usawa, ili kila aliyehitimu awe na fursa sawa ya kumiliki nyumba.
Kila Mkenya anayestahiki anahimizwa kuonyesha nia yake, kutembelea maeneo kutazama maonyesho ya nyumba, na kushirikiana na wafanyakazi wetu walio kwenye tovuti, ambao wako tayari kusaidia.
Kumekuwa na mjadala kuhusu mradi huu, huku Wakenya wengine wakiukaribisha lakini wengine wakisema Wakenya hawahitaji mradi kama huo kwa sasa, kuna mengine ya kupewa kipaumbele.
Machi 2023 akizindua mpango huu Rais Ruto aliangazia lengo la mpango huo katika kutoa nyumba za bei nafuu na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia kuunda nafasi za kazi.
“Mpango wa nyumba ni zaidi ya nyumba tu; ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa watu wetu, kwani ninazungumza zaidi ya nafasi za kazi 164,000 tayari zimeundwa, na ndio tunaanza," Rais Ruto alisema.