Wabunge nchini Uganda wanaitaka serikali iongeze juhudi za kujenga majengo yake katika mataifa hayo.
Uganda inatumia zaidi ya dola milioni 12.1( Shilingi biloni 44.4) kulipia majengo ya Balozi zake mbalimbali duniani kote.
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje, Ubalozi wa Uganda mjini Kigali umependekeza ununuzi wa moja kwa moja wa makazi rasmi kama suluhisho la muda mrefu la kupunguza gharama, zaidi ya dola milioni 1.5 ( shilingi bilioni 5.5) zinahitajika kwa ununuzi huo.
Ubalozi wa Uganda mjini Kigali pekee unahitaji dola za Marekani 8,000 (Shilingi milioni 29.6) kila mwezi kwa kodi ya makazi rasmi, hivyo dola 96,000 kila mwaka.
Idadi hii inakadiriwa kuongezeka hadi dola 10,000 kwa mwezi katika mwaka wa 2025.
Vile vile, ubalozi wa Uganda huko mjini New Delhi hutumia takriban dola 12,000 (Shilingi milioni 44.2) kila mwezi kukodisha ofisi za maafisa wake pekee.
Hii imesababisha wabunge kutoa wito kutaka Serikali iongeze juhudi za kujenga majengo yake katika mataifa hayo.
Wizara ya Mambo ya Nje imesema ubalozi wao mjini New Delhi unahitaji zaidi ya dola milioni 2.4 (Shilingi bilioni 9) kujenga kwenye ardhi iliyotengwa na serikali ya India ili kuepusha sehemu hiyo isikabidhiwe nchi nyingine.