Geingob, 82, alikufa mnamo Februari 4 katika hospitali ya Windhoek. Alikuwa akipatiwa matibabu ya saratani./ Picha : Ikulu TZ

Rais wa Kenya William Ruto ametoa wito kwa viongozi wa Afrika kupigania uhuru wa kiuchumi, kama njia pekee ya kuwakomboa kikamili vijana wa Afrika.

Rais Ruto, alikuwa miongoni mwa viongozi 18 kutoka nchi mbali mbali waliohudhuria mazishi ya rais wa Namibia aliyefariki Hage Geingob.

Katika hotuba yake aliwakumbusha hadhira kuwa marehemu rais Gengob alikuwa na azma ya kulikomboa bara kutoka utegemezi wa kiuchumi na kulikuza zaidi kwa misingi ya undugu.

''Tunajua kuwa Rais Gengob aliamini kuwa uhuru ni mradi, ambao unaendelea kufanyiwa kazi,'' alisema Rais Ruto. ''Lazima tufanyie kazi mradi huu, hasa wakati huu ili tuweze kujikomboa sio tu kwa lengo la kujitawala bali pia tukomboe chumi zetu ambazo zimegubikwa na madeni,'' aliongeza Ruto.

Udeni kwa usawa na haki

Pia Rais Ruto alisisitiza haja ya viongozi kuweka pamoja juhudi zao kukomboa vijana wa nchi zao na vizazi vijavyo kutokana na ukosefu wa ajira akisema kuwa vilikuwa vigezo muhimu katika utawala wa Rais Geingob na maono yake ya Afrika kwa jumla.

Kutokana na ushawishi wa marehemu Rais Gengob, Ruto alitoa wito kwa viongozi waliokuwepo ambao wanawakilisha makanda yote ya SADC, EAC na ECOWAS, kushirikiana chini ya mwamvuli wa AU kuhakikisha mataifa ya Afrika yanaingia udeni na wafadhili kwa misingi ya usawa na haki.

Ruto alisema kuna haja ya kuleta mabadiliko makubwa katika mifumo ya ukopaji ambapo itaondoa dhuluma upande wa Waafrika, kwa kuweka riba zinazostahiki na zisizowakandamiza wana bara hili.

Geingob, 82, alikufa mnamo Februari 4 katika hospitali ya Windhoek. Alikuwa akipatiwa matibabu ya saratani.

TRT Afrika