Mvua kali imesababisha mafuriko katika kijiji cha Kamuchiri cha Mai Mahiu / Picha: Reuters

Rais wa Kenya William Ruto, amefanya ziara maalumu katika mji wa Mai Mahiu na kuwafariji wananchi walioathiriwa na mafuriko makubwa yaliyotokea katika eneo hilo.

Katika salamu zake za rambirambi, rais Ruto ameahidi serikali yake kutoa msaada kwa waathirika.

Ziara ya Ruto ya kuwafariji walioathiriwa na mafuriko Mai Mahiu. / Picha: KBC

"Tutahakikisha watu wa Mai Mahiu wamepata msaada, watapewa chakula, madawa, blanketi na matresi (magodoro) ili tupunguze uzito ambao wako nayo," amesema rais Ruto.

"Kesho watasaidiwa kuondoka kwa muda muafaka, nguvu zote za serikali zitasaidia kuhakikisha kuwa watu wote wamepata makao mengine salama," Ruto aliwaahidi waathiriwa.

Aidha Rais Ruto ametoa saa 48 kwa wale wanaoishi pembezoni mwa mito kuotndoka maeneo hayo haraka iwezekanavyo.

Pia ameahidi kujengea nyumba wale waliopoteza makazi yao, na wale waliopoteza vitambulisho na nyaraka nyengine kurudishiwa.

Ruto atoa salamu zake za rambirambi kwa walioathiriwa na mafuriko. / Picha: Mai Mahiu

Hapo awali Mamlaka ya Rasilimali za Maji (WARMA) imeonya kwamba huenda kukatokea kwa mafuriko katika mabwawa ya Seven Forks kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

WARMA ilisema mabwawa ya kuzalisha umeme ya Seven Forks yamejaa na kuanza kumwaga maji kwenye mkondo.

Mamlaka ya Maji ilisema mabwawa kama Masinga, Kamburu, Gitaru, Kindaruma na Kiambeere yamepokea maji mengi kutoka Mlima Kenya na Abardare.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa WARMA Mohammed Shrurie alisisitiza kuwa agizo la kuhama mapema kwa wakaazi wanaoishi chini ya mto lilikuwa muhimu ili kuepusha hatari zinazoweza kusababishwa na mafuriko.

Mafuriko yatatiza usafiri na kuhangaisha wananchi nchini Kenya. / Picha: AFP

"Mabwawa mengi nchini yamejaa na hivyo kusababisha hatari ya mafuriko. Hadi tarehe 29/04/2024, mabwawa yote 7 ya kuzalisha umeme yanayojumuisha Masinga, Kamburu, Gitaru, Kindaruma yalikuwa yamefurika na kumwagika katika maeneo ya chini ya mto," alisema.

Shirika hilo lilitahadharisha zaidi kwamba mabwawa mengine katika maeneo ya mabonde ya Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Athi na Ewaso Ngiro Kaskazini yanakabiliwa na mafuriko, hivyo kuwataka wakazi wanaoishi karibu na mabwawa hayo kuwa waangalifu.

Baraza la mawaziri pia limeagiza raia wanaoishi ndani ya mifumo dhaifu ya ikolojia inayokabiliwa na mafuriko, maporomoko ya udongo, maporomoko ya ardhi na kando kando ya mito kuhama ndani ya saa 48 zijazo.

TRT Afrika