Rais William Ruto ameanza kufanya mabadiliko serikalini / Picha kutoka Ikulu 

Rais William Ruto wa Kenya amehutubia taifa lake akitoa mapendekezo ambayo anasema yametokea baada ya kuwasikiliza wananchi.

Rais amesema kuondoa Muswada wa Fedha wa 2024 kutapunguza bilioni 346 kutoka kwa malengo ya mapato ya mwaka huu. Ameongezea kuwa, pendekezo kwa bunge la kitaifa itakuwa ni kupunguzwa kwa bajeti ya bilioni 177 na serikali itakopa kufidia tofauti hiyo.

Fedha zilizokopwa ameelezea kuwa ni muhimu kulinda ufadhili wa maeneo muhimu kama vile kuajiri walimu wa shule za sekondari, wahitimu madakitari, miradi ya maziwa ya wakulima, mpango wa ruzuku ya mbolea, kulipa deni kwa wakulima katika sekta ya kahawa, na kuendeleza miradi ya sekta ya sukari katika ya sekta nyengine.

Maamuzi mengine

Wakati huo huo, Rais Ruto ametangaza kuwa jumla ya mashirika 47 ya serikali ambayo mengi yanafanya kazi zinazofanana yatafungwa. Wafanyakazi walioajiriwa huko watahamishwa wizara na mashirika mengine ya serikali.

Kuteuliwa kwa Makatibu Tawala Wakuu kumesimamishwa

Washauri wa seriklai kupunguzwa kwa asilimia 50.

Bajeti za ofisi za mke wa rais, mke wa naibu wa rais na mke wa waziri mkuu zimeondolewa.

Wafanyakazi wa serikali ni lazima sasa kustaafu wakiwa miaka 60 bila kuongezewa muda.

Ununuzi wa magari ya serikali nao umesimamishwa kwa miezi 12 isipokuwa kwa mashirika ya usalama.

Usafiri wa wafanyakazi wa serikali ambao si muhimu umesimaishwa.

Wafanyakazi wa serikali hawataruhusiwa kujihusisha na michango ya umma au harambee.

Rais William Ruto amesema atafanya mabadiliko mengine katika serikali hivi karibuni.

TRT Afrika