Utawala wa rais William Ruto umekumbwa na msukosuko kwa muda wa wiki mbili, huku vijana wa Kenya wakimtaka ajiuzulu. / Picha: AFP

Rais William Ruto wa Kenya amesema yupo tayari kuongea na vijana katika mtandawo wa X, ambao umeibuka kama jukwaa la majadiliano nchini humo kuhusu kampeni dhidi ya uongozi wa Rais Ruto.

"Nasikia vijana wanasema hawataki jukwaa la sekta nyingi. Labda tuwe na maongezi na Rais kwenye X. Niko wazi kuwa na majadiliano na vijana kwenye jukwaa ambalo wanafurahia. Ikiwa wanataka nishirikiane nao kwenye X, nitakuwepo," Rais amesema tarehe 5 au sita majadiliano haya yatafanyika.

Utawala wa Ruto umekumbwa na msukosuko kwa muda wa wiki mbili, huku vijana wa Kenya wakimtaka ajiuzulu. Maandamano yameongozwa na vijana maarufu Gen Z kwanza wakitaka muswada wa fedha 2024 utupiliwe mbali na sasa wanadai rais ajiuzulu.

Rais William Ruto amesema wanajeshi hawatakuwa mitaani, huku nchi ikiendelea kushutumu maamuzi yake ya kutumisha wanajeshi kwa ajili ya maandamano.

"Vikosi vya wanajeshi, KDF, havitakuwepo barabarani vinakuja tu kama suluhu ya mwisho. Ikiwa maandamano yatakuwa ya amani nawaahidi polisi watakuwepo kuwalinda waandamanaji," Rais Ruto alisema katika mahojianio na waandishi wa habari

"Lakini polisi pia watakuwepo kuhakikisha kwamba wahalifu wanaokuja kuharibu maofisi, kupora mali nao watashughulikiwa. Hiyo ni dhamira yangu. Sote tufanye kazi kwa mujibu wa sheria," Rais ameongezea.

Katika mahojiano na waandishi wa habari , rais sasa anataka kufungua ofisi yake kwa vijana, ambao amelalamikiwa kwa kushindwa kuwashirikisha ipasavyo.

"Marafiki wazuri, vijana wa taifa letu, wanangu wa kiume na wa kike walioniunga mkono kushinda uchaguzi nawasikia," amesema.

"Niliona bwana mmoja wa kijijini kwangu alikuwa anasema 'rais ametuangusha watoto wengi kijijini hapa hawapati ajira ndio maana wanaenda nje ya nchi.' Hakujua, rafiki yangu wa kijijini kwangu kwamba wenzake 500 kwa kweli ni sehemu ya mpango wangu kuhusu usafirishaji wa wafanyikazi," Rais Ruto amesema.

Waandishi wa habari walimuuliza rais Ruto kuhusu mauaji ambayo yalifanywa na maafisa wa polisi wakati wa maandamano. Shirika la Taifa la Haki za Binadamu. KHRC imesema watu 23 wameripotiwa kuuawa kwa risasi au majeraha, katika wiki mbili zilizopita za maandamano katika sehemu tofauti za nchi.

"Kila mtoto, kila mama anahisi sawa wakati mzazi wao anashambuliwa. Ndivyo ilivyo, lakini nikuulize, vipi kuhusu watoto wa wale ambao wamepoteza maisha kwa sababu ya uhalifu wa wengine, hawajisiki sawa? Hivyo tunatakiwa tuwe nchi ya utawala wa sheria kwani uhalifu upo pande zote," Rais amesema.

"Wanaoheshimu sheria lazima walindwe na sheria wale wasioheshimu sheria lazima wakumbane na nguvu zote za sheria. Kuna watu wengi katika maandamano haya wamepoteza maisha leo watoto wao wanalia, leo wake zao wanatokwa na machozi, kwa sababu hawajui jinsi ya kukabiliana na kesho. Biashara zao zimefutwa mapato yao yameharibiwa," Rais Ruto ameelezea.

"Sasa hivi nimekwambia biashara yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4 (zaidi ya dola Milioni 18.6) imeharibiwa na hivi ninavyozungumza na wewe kuna familia zinatokwa na machozi, kuna familia hazijui jinsi ya kukabiliana na kesho," Ruto aliongezea.

Hali nchini Kenya bado haijatulia huku vijana wakiapa kuendela maandamano kupinga uongozi wa rais Ruto.

TRT Afrika