Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alipenda sana kufanya mazoezi wakati wa uhai wake./Picha: Wengine

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Novemba 26, 1993 Hayati Ali Hassan Mwinyi, alikuwa ni sehemu ya mamia ya watazamaji waliofurika katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), kushuhudia mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika(CAF) kati ya Simba ya Tanzania na Stella Abidjan kutoka Ivory Coast.

Mzee Mwinyi, wakati huo alihudhuria mechi hiyo kama mgeni rasmi, wakati huo akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mchezo huo wa fainali, ulikuwa ni marudio ya mechi ya kwanza iliyofanyika nchini Ivory Coast baada ya timu hizo mbili kutoka suluhu ya bila ya kufungana.

Kama yalivyokuwa mategemeo ya Watanzania wengi kipindi hicho, Rais Mwinyi pia alikuwa na hamu ya kuona Simba inatwaa ubingwa huo, ambao ungeifanya timu hiyo kuwa ya kwanza kutoka Tanzania kushinda taji hilo kubwa barani Afrika.

Hakika ilikuwa mechi kubwa, na taifa lote liliungana na kuwa kitu kimoja, kila mmoja akiiombea Simba, iliyokuwa ikifundishwa na Abdallah Kibadeni itwae kombe hilo.

Ikumbukwe kuwa, wachezaji wa Simba walaahidi zawadi nyingi kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwemo ahadi ya kununuliwa magari aina ya KIA, kutoka kwa aliyekuwa mfadhili wao, Azim Dewji.

Ndoto zayeyuka

Hata hivyo, mabao mawili yalifungwa na Boli Zozo wa Stella Abidjan, yalitosha kuzima ndoto za watanzania kutwaa kombe hilo, na kuuacha uwanja wote katika simanzi kubwa.

Kama ishara yake ya kusitishwa na matokeo yale, Rais Mwinyi alitamka wazi kuwa, katika soka, "Tanzania ni sawa na kichwa cha mwendawazimu", na kwamba kila mtu anaweza kujifunzia kunyolea.

Kauli hiyo, ni kama iliendelea kuakisi ukweli halisi wa mambo, kwani kwa miaka mingi baada ya hapo, timu za kutoka Tanzania haikufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

Hata hivyo, miaka 25 baadaye, Mzee Rukhsa, kama alivyojulikana na wengi alitengua kauli yake.

Mzee Mwinyi alifuta kauli hiyo alipokuwa anahudhuria ugawaji tuzo za Simba ‘Mo Awards’, ambapo alionekana kufurahia tukio hilo.

“Ndugu zangu, kuanzia leo, nafuta kauli yangu, najua mnaikumbuka kwahiyo naiondoa kabisa siku ya leo,” alisema maneno hayo kisha akaomba kuondoka ukumbini hapo baada ya shughuli hiyo iliyofanyika Dar es Salaam.

TRT Afrika