Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika/ picha Reuters 

Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kiongozi wa Chama cha Upinzani Azimio nchini Kenya, Raila Odinga ametangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

"Nimekuwa nikishauriana sana. Nadhani kama niko tayari kutumikia bara la Afrika. Afrika inastahili ubora zaidi. Niko tayari kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika," Raila Odinga amesema katika mkutano na waandishi wa habari jijini Nairobi nchini Kenya.

Nafasi hiyo kwa sasa ipo chini ya Moussa Faki Mahamat ambae ni raia wa Chad, ambae aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo. Awamu yake ya pili ya uongozi inakwisha mwaka huu 2024.

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ameuunga mkono uamuzi huyo wa Raila Odinga, ambae pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya.

"Sina shaka kwamba rafiki yangu huyu ndiye mtu bora kuchukua jukumu hiyo. Ikiwa kanda ya Afrika Mashariki itamuunga mkono, basi ataweza," Obasanjo amesema akiwa na Odinga katika mkutano huo wa waandishi wa habari.

Mwaka 2017 Kenya ilijaribu kupata nasafi hiyo ya juu kupitia mwanasiasa wake Amina Mohammed, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya wakati huo.  Picha Reuters.

Hii sio mara ya kwanza kwa Kenya kugombea nafasi hiyo ambayo ni kubwa katika bara la Afrika. Mwaka 2017, Kenya ilijaribu kupata nasafi hiyo ya juu kupitia mwanasiasa wake Amina Mohammed, aliyekuwa wakati huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya.

Hata hivyo, Kenya ilishindwa na Chad iliyowakilishwa na Moussa Faki Mahamat.

Raila amewahi kutoa huduma ya kibara.

Aliteuliwa kuwa Mwakilishi Mkuu wa Maendeleo ya Miundombinu katika Tume ya Umoja wa Afrika mwaka wa 2018. Majukumu hayo yalikwisha Februari 2023.

Ili kupata kiti hiki, marais wa nchi za Afrika hupiga kuwa ya siri. Mgombea anahitaji kupata angalau theluthi mbili ya kura, kura 36, ​​ili kutangazwa mshindi.

Kazi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ni ipi?

Nchi ambayo inataka kiti hiki hupendekeza nia yake na kugombea na kumteuwa mtu ambaye atagombea nafasi hiyo.

Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Umoja wa Afrika ni Moussa Faki Mahamat kutoka Chad/ Picha: AFP

Ni lazima nchi husika kufanya kampeni katika nchi tofauti kwani uchaguzi hufanywa na marais na viongozi wa nchi.

Mwenyekiti wa Tume ya AU huchaguliwa na marais wa Afrika kwa kipindi cha miaka minne. Anaweza kugombea tena kiti hiki mara moja tena.

Mgombea anahitaji kupata angalau theluthi mbili ya kura, hiyo ni angalau kura za marais 36, ​​ili kutangazwa mshindi.

Kazi ya Mwenyekiti wa Tume ya AU

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika ni Afisa Mkuu Mtendaji, mwakilishi wa kisheria wa AU na Afisa Mkuu wa Uhasibu wa Tume.

Majukumu yake ni pamoja na

  • Usimamizi wa fedha za Tume ya Afrika
  • Kuchukua hatua zinazolenga kukuza na kutangaza malengo ya AU na kuimarisha utendaji wake
  • Kuwezesha utendakazi, kufanya maamuzi na kuripoti mikutano yote ya mashirika ya AU, na kuhakikisha ulinganifu na uwiano na sera, mikakati, mipango na miradi ya AU iliyokubaliwa.
  • Kushauriana na serikali za nchi wanachama wa AU, taasisi nyingine na mashirika ya kikanda kuhusu shughuli za AU.
  • Kuiwakilisha kidiplomasia muungano wa AU.
  • Utayarishaji wa bajeti wa AU akishirikiana na kamati ya wawakilishi wa nchi za Afrika katika AU yaani mabalozi.
  • Kufanya kazi kama hifadhi kwa mikataba yote ya AU na OAU na vyombo vya kisheria.

Orodha ya wenyeviti wa zamani wa Tume hiyo

2017– hadi sasa - Moussa Faki Mahamat, Chad

2012–17- Princess Dlamini Zuma, Afrika Kusini

2008–12 - Jean Ping, Gabon

2003-08 - Alpha Oumar Konaré, Mali

2002–03 (miaka ya mpito ya OAU hadi AU) - Amara Essy, Ivory Coast

TRT Afrika