Nafasi hiyo kwa sasa ipo chini ya Moussa Faki Mahamat ambae ni raia wa Chad, / Picha: AFP

Kiongozi wa upinzani nchin Kenya Raila Odinga ameendelea kulimbikiziwa sifa kutoka ndani na nje ya nchi kuelekea kuungwa mkono kwake kuchukua wadhifa wa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika AU.

Jumamosi, chama tawala nchini Kenya kilielezea kumuunga mkono bwana Odinga huku maafisa wakinukuliwa kusema kuwa ni mzalendo mwenye maono ya Afrika na anaweza kuongoza Umoja huo.

Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Kenya UDA, Cleophas Malala, akizungumza na wanahabari siku ya Jumamosi, alimsifia kiongozi huyo wa chama cha Azimio la Umoja Kenya akimtaja kuwa "mkereketwa wa kweli wa Afrika."

"Tunakaribisha uamuzi wa Raila kuchukua nafasi ya AU,'' alisema Malala. ''Raila ni kinara wa Afrika anayestahili nafasi hiyo kulingana na mchango wake katika bara hili, na atachangia pakubwa umoja wa Afrika," alisema Malala.

Wiki iliyopita Raila alitangaza nia yake kuwania uenyekiti wa Umoja wa Afrika, hatua ambayo imepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa washirika wake na mahasimu wake wa kisiasa.

Chama kingine cha upinzani nchini Kenya ANC, kilisema Jumapili kuwa kinamuunga mkono Raila kuwa mwenyekiti wa AU kikitaja hatua hiyo kama hatua kubwa ya kidiplomasia kwa Kenya na Afrika Mashariki.

"Tunapongeza juhudi za kidiplomasia za Kenya katika Mkutano wa Wakuu wa AU unaoendelea Addis Ababa, unaoongozwa na Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, na tunaamini kuwa wakati umefika kwa Kanda ya Afrika Mashariki kuongoza tume ya AU," ilisema ANC katika taarifa.

Raila Odinga pia ameungwa mkono na Rais mstaafu wa Nigeria Olesogun Obassanjo ambaye alielezea imani yake kwa Odinga kuendeleaza utangamano wa Afrika.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ni mkuu wa kuteuliwa wa Umoja wa Afrika (AU) anayepigiwa kura na Bunge la Wakuu wa Nchi na Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja. Cheo hiki kinazunguka kati ya maeneo matano ya bara. Mgombea lazima achaguliwe kwa makubaliano au angalau thuluthi mbili ya kura na nchi wanachama.

Nafasi hiyo kwa sasa ipo chini ya Moussa Faki Mahamat ambae ni raia wa Chad, ambae aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo. Awamu yake ya pili ya uongozi inakwisha mwaka huu 2024.

TRT Afrika