Mwanariadha wa marathon kutoka Uganda Rebecca Cheptegei na mumewe wamelazwa katika hospitali kuu ya Eldoret nchini Kenya, kufuatia tukio la kuchomwa moto unaoaminiwa kutokana na mzozo wa kinyumbani.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi wa eneo hilo, tukio hilo lilitokea mwendo wa saa nane mchana Jumapili, ambapo Dickson Ndiema, mumewe waliotengana kwa muda, alipomsubiri nyumbani akitoka kanisani na kumwagia petroli na kisha kuwasha moto.
Cheptegei aliokolewa na majirani waliomkimbiza hospitalini ambapo anapokea matibabu ya kuungua sehemu mbali mbali mwilini.
Mume wake Ndiema pia alipata majeraha ya kuungua baada ya moto aliyowasha kumchoma pia.
Ripoti hiyo inafichua kwamba wawili hao wamekuwa katika mzozo kwa muda mrefu.
"Watu hao wawili walikuwa wanandoa ambao mara kwa mara walikuwa na migogoro ya kifamilia ambapo waligombania kiwanja na nyumba," ripoti hiyo yasema.
Kamanda mkuu wa polisi wa kaunti ya Uasin Gishu amethibitisha tukiuo hilo n akusema kuwa polisi wameanza uchunguzi.
Cheptegei alishiriki kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris ambapo alimaliza wa 44 katika mbio za marathon za wanawake.
Matokeo bora zaidi ya mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 33 kufikia sasa ni katika mbio za Padova Marathon mnamo 2022 ambapo alitumia 2:31:21 kumaliza wa kwanza.
Alishinda pia dhahabu kwenye Mashindano ya Dunia ya Milima na Trail Running huko Chiang Mai, Thailand mnamo 2022.