Polisi Uganda watibua shambulio la kigaidi dhidi ya kanisa na kumkamata mshukiwa mmoja

Polisi Uganda watibua shambulio la kigaidi dhidi ya kanisa na kumkamata mshukiwa mmoja

Washukiwa wengine watatu wanatafutwa wanaoaminiwa pia walikuwa na njama ya kushambulia maeneo mengine mjini Kampala
Uganda police

Polisi nchini Uganda walisema siku ya Jumapili walimzuilia mwanamume mwenye umri wa miaka 28 akiingia kanisani katika mji mkuu wa Kampala akiwa na kilipuzi alichopanga kutumia kushambulia huko.

''Tulipata maelezo ya kijasusi mapema ashubuhi kuwa kuna njama ya kushambulia maeneo ya maombi leo,'' amesema msemaji wa polisi jiji la Kampala, Patrick Onyango.

''Vile vile tulipata taarifa kuwa mmoja wa washukiwa hao alikuwa tayari ameshafika mjini. Kwa hiyo tulimfuatilia na tukamkamata,'' aliongezea Onyango.

Polisi wamesema kuwa mshukiwa huyo wa miaka 28, alikutwa na bomu lililokuwa ndani ya kidishi cha chakula na waliweza kulitawanya.

''Mshukiwa huyo alizuiliwa alipokuwa akikaribia kuingia katika kanisa la Pentecostal, Lubaga Miracle Centre, katika kitongoji cha Lubaga kusini mwa Kampala,'' alisema Patrick Onyango.

Bado hakuna maelezo iwapo mshukiwa huyo alikuwa akifanya kazi na kikundi chochote kinachojulikana, japo kumekuwa na mashambulio awali ambazo zilihusishwa na wanamgambo wa ADF, walio na uhusiano na kundi la kigaidi lijulikanalo kama Daesh.

Kwa mujibu wa idara ya upelelezi ya Uganda, mamlaka zilikuwa zikiwasaka wanaume wengine watatu wanaoaminika kutumwa kwenye misheni kama hiyo ya ulipuaji wa mabomu kwingineko nchini Uganda.

Hapo awali ADF lilikuwa kundi la waasi wa Uganda lakini lilitimuliwa zaidi ya miongo miwili iliyopita na kukimbilia katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako limekuwa na makao yake.

TRT Afrika