Uganda Tiktok

Vijana wawili wamenaswa na polisi nchini Uganda kwa kosa la kusambaza video kuonyesha uhalifu wa mtandao na teknolojia na utumiaji mbaya wa kompiuta.

Msemaji wa kitengo cha polisi cha Kampala Metropolitan SP Patrick Onyango, amesema kuwa baada ya uchunguzi vijana hao walikiri kurekodi video hiyo ambayo imesambaa sana mtandaoni.

''Baada ya kuwahoji, walikiri kuwa walirekodi video kutafuta likes katika mtandao wa kijamii kama vile TikTok,'' amesema Onyango. '' Japo walitengeneza video kwa ajili ya likes ya mtandao wa kijamii, tunawapeleka mahakamani na tutawafungulia mashtaka,'' aliongeza Onyango.

Video ya vijana hao wakionyesha namna wanavunja password za simu kwa urahisi, imesababoisha ghadhabu mtandaoni huku watazamaji wengi wakitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Wakaazi wengi wa mji mkuu Kampala wamesema kuwa visa vya wizi wa simu vimeongezeka hasa kutoka kwa wabakuraji wa barabarani.

Katika video yao, mmoja wa vijana hao alidai kuw amwanafunzi wa somo la ICT katika chuo mjini Kampala, nao polisi walithibitisha hilo kuwa kweli.

''Tumegundua kuwa ni kweli ni wanafunzi wa chuo. Sasa tunachunguza zaidi kujua iwapo madai waliyotoa katika video yao pia ni kweli,'' Onyango aliambia waandishi wa habari.

Serial number za simu huwasaidia polisi kuzifuatilia na kunasa kutoka kwa wezi lakini iwapo zimevurugwa, basi inakuwa vigumu kuzitambua.

Kwa mujibu wa data za polisi Uganda, zaidi ya simu za mkononi za thamani ya dola milioni mia moja thelathini zimeibwa mwaka jana pekee ikiwa ni ongezeko la 6.8% kulingana na 2002.

''Tutawashitaki mahakamani, ili iwe funzo kwa wengine wanaofanya au wana nia ya kufanya makosa kama hayo. Kuwa sio tu kwa ajili ya kujifurahisha mtandaoni,'' alisema Onyango. ''Ukijifurahisha mtandaoni kumbuka kuwa kuna sheria itakayokunasa,'' aliongeza Onyango.

TRT Afrika