Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Mkuu wa Huduma ya Taifa ya Polisi imesema, kuwa kutokana na taarifa za kiintelijensia ilizopata, kwamba kuna makundi ya uhalifu ambayo yanapanga kujipenyeza, na kuharibu maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika hii leo, hivyo kuhatarisha usalama wa waandamanaji.
“Wakati mnaandamana, tunawasihi kuandamana kwa utulivu, na kujihami. Tafadhali, toa ushirikiano na polisi kuhakikisha usalama wako,” imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Douglas Kanja Kirocho, ambae anakaimu nafasi ya Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya.
Wakati huo huo, tayari maandamano yameripotiwa katika maeneo kadhaa nchini Kenya, ikiwemo jiji la Nairobi, Bungoma, Kisumu, Kakamega.
Maandamano haya ni muendelezo wa maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea nchini humo, awali yaliyotaka kutupiliwa mbali kwa mswada tata wa fedha.
Hata hivyo, licha ya kilio chao kusikizwa na Rais Ruto ambae alikataa kuusaini na hatimae kuutupilia mbali, lakini kizazi cha Gen Z kilikuja na matakwa mengine na kumshikiza Rais Ruto kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.
Wiki iliyopita, kwa mara ya pili katika historia ya nchi hiyo, Wakenya walishuhudia rais wa awamu wa tano William Ruto akiwafuta kazi mawaziri wake wote pamoja na Mwanasheria Mkuu.
“Nimeanza sura mpya na nitaunda serikali mpya. Ninaomba mniombee ili nipate watu ambao watanisaidia kutimiza ahadi nilizotoa kwa Wakenya,” amesema Rais Ruto katika moja ya hotuba zake kwa Taifa.
Kitendawili cha baraza jipya
Wakati Rais Ruto akijitafakari jinsi ya kusuka upya baraza lake la mawaziri, kizazi cha Gen Z na Wakenya kwa ujumla wanasubiri kwa hamu kuona safu yake mpya.
Huku wakitoa baadhi ya vigezo wanavyotaka vizingatiwe katika uteuzi. Miongoni mwa vigezo hivyo ni pamoja na:
- Wawe watendaji zaidi kuliko wanasiasa
- Wasiwe na tuhuma za ufisadi
- Vijana kuanzia miaka 25-60
- Wasiwe na uhusiano wa kifamilia, kisiasa, au kirafiki na rais
- Wasiwe wamewahi kuhudumu kama mawaziri katika serikali zilizopita
Jinamizi la mauaji
Wakati haya yakijiri, taifa hilo la Afrika Mashariki, linaloaminika kuwa na uchumi imara, linakabiliwa na simanzi kufuatia kupatikana kwa miili kadhaa ya watu waliouawa na miili yao kutupwa katika dampo nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Ingawa serikali tayari imeahidi kuchunguza mauaji hayo, baada ya kukamatwa kwa Collins Jomaisi Khalisia anayedaiwa kuwa muhusika mkuu.