Takriban watu 20 wamefariki baada ya mashua kuzama katika maji ya Uganda, Ziwa Victoria siku ya Jumatano.
Polisi Uganda inasema watu 34 wanadaiwa walikuwa katika boti hiyo.
Polisi imeripoti kuwa watu tisa wameokolewa katika ajali hiyo iliyotendeka saa kumi na moja asubuhi.
"Juhudi za uokoaji zinaendelea huku timu za Wanamaji wa Polisi, Kitengo cha Ulinzi wa Uvuvi cha UPDF na jumuiya ya eneo kwenye maji ikijaribu kuwatafuta watu waliopotea, " Patrick Onyango, msemaji wa jeshi la polisi jijini Kampala amesema.
Alisema operesheni unaendelea ili kuwapata watu watano waliopotea.
Chanzo cha ajali kimehusishwa na upakiaji kupita kiasi na hali mbaya ya hewa.
" Boti hiyo ilikuwa imebeba mifuko ya mkaa, chakula, samaki wa biashara miongoni mwa mengine," Onyango ameongeza.
"Tunatoa wito kwa wananchi wanaosafiri majini kuvaa jaketi za kuokoa maisha kila mara na kutopakia vyombo vyao kupita kiasi."
John Wandera, mvuvi ambaye alikuwa miongoni mwa waliookoa walioathirika, alisema kuwa boti hiyo ilipinduka kutokana na upepo mkali.
Maafa zaidi Ziwa Victoria
Mnamo Julai 5, watu watano walikufa wakati mitumbwi ilipopinduka katika ziwa moja katika wilaya ya Mukono.
Ajali ya boti Uganda inakuja siku moja tu baada ya ajali nyingine kutokea Tanzania, tarehe Mosi Agosti.
Mitumbwi miwili iliyokuwa imebeba waumini 28 wa Kanisa Takatifu la Mungu wa Kiroho (KTMK) ilizama ziwani ambapo watu 14 waliokolewa, wakiwemo watoto 11 walihusika katika ajali kwenye ufuo wa Ziwa Victoria.