Katiba inatoa maagizo kuwa rais mstaafu apate rasilimali aina tofauti ya ofisi yake/ Picha:  Ofisi ya rais wa Nne Kenya  

Rais wa Kenya William Ruto amempigia simu rais wa zamani Uhuru Kenyatta kuhusu ripoti kutoka kwa ofisi ya Kenyatta kuwa hapati rasilimali anazofaa kama rais mstaafu.

Kumekuwa na mvutano kwa muda sasa kati ya ofisi ya rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta na serikali ya sasa inayoongozwa na William Ruto.

Ofisi ya Kenyatta imedai kuwa haipati rasilimali ambazo katiba inasema inafaa kupata.

Ofisi yake imethibitisha kuwa Kenyatta ameshapokea malipo ya jumla ya $370,656 (shilingi milioni 48) kama bakshishi na kuwa yeye hupokea malipo yake kila mwezi na bima ya matibabu.

Maswala ya utata ni yapi?

Kanze Dena ambaye ni Mkuu wa mawasiliano wa rais wa zamani Uhuru Kenyatta anasema ofisi ya rais haijapata fedha zote ambazo zimetajwa katika bajeti.

Akidai kuwa ni takriban 4.4% ya bajeti yote ambayo ofisi hiyo imepokea. Haya ni malipo ya kabla ya mshahara na bima ya matibabu.

"Katika mwaka 2022/2023 bajeti ya bunge ilitengewa afisi hii ilikuwa shilingi milioni 655. Kufikia sasa ofisi inaweza tu kuthibitisha utumiaji wa 28 million zilizosambazwa katika malipo ya posho ya usafiri wa ndani na usafiri wa ndani pamoja na kuwezesha safari 2 ambayo imefanyika kufikia sasa," Dena amesema.

Kanze Dena mkurugenzi wa mawasilianokwa ofisi ya rais wa zamani wa Kenya asema ikulu haiwapi rasilimali zinazofaa/ Picha: Ofisi ya rais wa Nne wa Kenya 

Hata hivyo maafisa hao wamethibitisha wanapata misharaha na bima ya afya.

"Suala lingine ni kwamba Ikulu huchagua njia ya mdomo ya mawasiliano kuhusu masuala rasmi au kuchagua kutojibu barua zinazotolewa na ofisi hii. Hii ni pamoja na kusainiwa upya kwa mikataba ya wafanyakazi 2," Dena ameongezea.

Kandarasi yake Dena na afisa mwingine haijafanywa upya bado.

"Sheria ya Kustaafu ya Rais inabainisha kuwa Rais wa zamani anapaswa kuwa na wafanyakazi 34. Tayari, 33 wako ofisini. Sheria pia inabainisha kuwa wanaofanya kazi katika Ofisi ya Rais Mstaafu ni lazima wawe watumishi wa umma. Kuhusu Bw. George Kariuki na Bi Kanze Dena, majina yao hayajatumwa kwa Msimamizi wa Ikulu na Rais mstaafu ili kushughulikiwa,"

Ofisi ya Kenyatta pia imelalamika kuwa rais wa zamani hajapata haki ya safari nne za kimataifa.

" Sheria inasema kuwa Rais wa zamani ana haki ya safari 4 za kimataifa. Tangu kustaafu hadi leo ni safari 2 tu kama hizo zimeheshimiwa. Kutoka kwa Waandishi wa habari tulipata kujua kwamba suala ni ukubwa wa ujumbe jambo ambalo liliwasilishwa kwa maneno. Ikiwa kweli suala lilikuwa ukubwa wa wajumbe, kwa nini wasishughulikie hoja 10 kama inavyoshauriwa na Mambo ya Nje?" Dena amesema katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Ofisi ya Kenyatta pia inadai kuwa ilitaka ofisi ambayo Kenyatta alichjagua na sio ambayo seriklai iliamua kumpa.

"Barua rasmi iliandikiwa ikulu kuomba kuthaminiwa kwa afisi hiyo ambayo ilitambuliwa na Rais Kenyatta kuwa inafaa kwake kutekeleza majukumu yake. Hata hivyo, ofisi hiyo haikupokea majibu kuhusu suala hilo kwa ikulu," Dena amesema.

Lakini serikali ya Rais Ruto imesema serikali haiwezi kupia kodi kwa nyumba kwa oifisi ambayo ipo katika nyumba ya Kenyatta.

"Katika mwaka 2012/2013, serikali ilinunua ofisi ya Rais mstaafu. Ofisi hii iko Nyari, Nairobi. Hii ndiyo ofisi ambayo marehemu Rais Mwai Kibaki aliitumia kwa miaka 9, kati ya 2013 na 2022. Kwa hivyo, ni ofisi inayofaa kwa Rais yeyote mstaafu," msemaji Mwaura amesema.

" Kwa kuikataa ofisi hii na kupendelea serikali ipangishe nyumba yake binafsi, Rais Mstaafu wa Tatu anaialika serikali kukiuka sheria, kanuni na taratibu za manunuzi. Rais Mstaafu anataka kuwa mwenye nyumba na mpangaji kwa wakati mmoja," Mwaura amedai.

Haya ni baadhi tu ya malalamiko kutoka kwa ofisi ya rais wa nne wa Kenya.

Baada ya mvutano huu wa hadharani kwa vyombo vya habari, ssemaji wa rais William Ruto anasema Ruto ameongea na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

"Leo asubuhi, Rais Ruto alikuwa na mazungumzo na mtangulizi wake ofisini, Rais wa nne, Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu wasiwasi kuhusu kuwezesha utendakazi wa afisi ya Rais mstaafu," Hussein Mohammed msemaji wa Ikulu amesema katiak akaunti yake ya X.

"Kwa hivyo, Rais Ruto ameunda timu, inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, kushughulikia mara moja masuala yote yaliyoibuliwa, ikiwa ni pamoja na eneo la ofisi ya Rais mstaafu na wafanyikazi," Mohammes ameongezea.

TRT Afrika