Mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine uliingia katika mwaka wake wa pili wiki chache zilizopita. Mzozo huo unaendelea kuleta ugumu wa maisha kwa wakazi barani Afrika huku ufanisi wa hatua zilizochukuliwa na Serikali kupunguza athari za usambazaji wa chakula zikikabiliwa na mtihani mgumu.
Kwa bara ambalo uagizaji wa chakula nje ulikua zaidi ya dola bilioni 45 kila mwaka licha ya kuwa na asilimia 60 ya ardhi yenye rutuba isiyolimwa na nguvu kazi ya vijana, ilikuwa ni suala la muda athari zake kujitokeza pale uhaba wa chakula utakapoikumba dunia nzima. Mwanzoni, lawama zilitupiwa kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) na sasa zimeelekezwa kwa vita hio.
Ukweli ni kwamba, ni nchi chache sana Afrika, ikiwa zipo, zilikuwa na hifadhi ya chakula cha kutosha watumiaji wake japo kwa muda mfupi tu, hasa baada ya janga la UVIKO-19 kupita ambalo lilivuruga mfumo usambazaji bidhaa kimataifa na kupelekea bei ya mafuta, gesi na bidhaa zingine kupaa.
Kwa uzalishaji wa ndani wa mazao na mifugo ambao unategemea sana pembejeo, mbolea na malighafi nyingine kutoka nje, vita hio imesababisha kuongezeka kwa gharama za uzalishaji bidhaa za vyakula na bidhaa za viwandani, na kuumiza zaidi walaji wa kipato cha chini na maskini zaidi.
Hali hio imefichua udhaifu wa mifumo ya chakula ndani ya mataifa hayo, na kikubwa zaidi, iliziacha nchi zikiwa hazina kitu cha kuonyesha licha ya ahadi za miaka mingi kuhusu uwekezaji kwenye sekta kilimo ili kuongeza usambazaji wa ndani wa bidhaa muhimu za chakula na bidhaa za kilimo.
Pia imeweka bayana wasiwasi wa muda mrefu juu ya kushindwa kwa viongozi kuheshimu ahadi chini ya Azimio la Malabo la mwaka 2014, ambapo bara la Afrika liliazimia kutenga angalau asilimia 10 ya bajeti ya Serikali katika kilimo ili kutokomeza njaa na umaskini katika nchi zao.
Kama hali inavyojionyesha sasa, miaka tisa baadaye, ni nchi moja tu - Rwanda -- iko kwenye njia ya kufikia malengo ifikapo 2025.
Nchi nyingine tatu ambazo zilikuwa zikipiga hatua vizuri kufikia malengo, zilianguka mwaka 2019, kulingana na ripoti ya mapitio ya kila baada ya miaka miwili iliyochapishwa na Umoja wa Afrika (AU) mwezi Machi 2022.
Ripoti hiyo imetokana na zoezi la upimaji uwajibikaji linalotekelezwa na shirika ambalo hufuatilia maendeleo ya Nchi wanachama katika kutekeleza Azimio la Malabo.
Licha ya kupiga hatua nzuri, Rwanda, kama Zimbabwe na Ghana, ni miongoni mwa nchi 10 bora zilizo na mfumuko wa bei wa juu zaidi wa bei ya chakula ulimwenguni kulingana na tathmini ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia.
Rwanda pia imekuwa na viwango vya udumavu kwa asilimia zaidi ya 30.
Kwa ujumla, kwa sababu ya misukosuko ya zamani na migogoro inayoendelea, juhudi za Serikali katika bara hilo hazitoi matumaini makubwa ya kumaliza umaskini na njaa katika siku zijazo labda tu kama zitaweka kipaumbele katika uwekezaji wa kilimo, kuchochea uzalishaji wa ndani na urahisi wa biashara ya pembejeo na mazao ya kilimo ndani na nje ya mipaka yao.
Huku athari za mzozo wa Urusi-Ukraine zikizidi kuumiza maisha ya mamilioni ya kaya kwenye bara hilo mwaka mmoja baadaye, udhaifu uliopo unadhoofisha uwezo wa mataifa kuzalisha chakula na kulisha idadi ya watu inayoongezeka. Bara la Afrika lina theluthi moja (milioni 283) kati ya watu milioni 850 duniani wenye tatizo la njaa.
Viongozi wa Kiafrika waliokutana katika mkutano uliopewa jina la 'Lisha Afrika: Uhuru wa Chakula na Ustahimilivu' uliofanyika Dakar, Senegal, walifahamu kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka zaidi ikiwa haitadhibitiwa.
Mkutano huo uliwezesha bara la Afrika kukusanya ufadhili wa dola bilioni 50 ili kukabiliana na uhaba wa chakula.
Hatua za kimakusudi za Serikali katika bara hili kimsingi zimelenga kutoa ruzuku kupunguza gharama za mafuta, mbolea, mafuta ya kupikia, nafaka na bidhaa zingine zinazohitajika kama pembejeo za kilimo au malighafi kwa uzalishaji, sambamba na kuchunguza vyanzo mbadala vya kuagiza kutoka nje. Hata hivyo, hatua hizi zimefanya kidogo kupunguza shida za watumiaji kwenye soko hadi sasa.
Uchumi wa Kiafrika unashindwa kudumisha ruzuku kwa vile haziwezi kuwekwa kwa bidhaa zote ambazo gharama zake zinawashinda watu wengi wa kipato ya chini na maskini.
Mateso hayo yanazidishwa na hali mbaya ya hewa kama vile ukosefu wa mvua na ukame ambao umeathiri pato la kilimo cha msimu katika maeneo mengi barani humo.
Wanasiasa lazima waondoke kwenye kasumba ya kutaka matokeo ya haraka kwa shida ya chakula na lishe inayoendelea. Wanatakiwa kubuni njia za muda mrefu za kujitoa katika hali hiyo na kujenga ustahimilivu kwa majanga mengine.
Juhudi na raslimali sasa ziwekezwe katika mipango ya ndani ambayo inasaidia kukabiliana na majanga ya njaa ya sasa na ya baadaye, hasa ile inayochochea uzalishaji wa mazao na mifugo, wakati huo huo kuondoa vikwazo vya biashara kati ya nchi na nchi ili kuruhusu wakulima kubadilishana na kufanya biashara katika bidhaa za chakula kwa urahisi.
Biashara ya ndani ya bara inayokuzwa chini ya soko huria la biashara Afrika (AfCFTA) ni hatua katika mwelekeo sahihi.
Juhudi kama vile Umoja wa Afrika (AU) ziliongoza uanzishwaji wa vitovu vya viwanda vya kilimo katika maeneo yote barani ili kuongeza usambazaji wa bidhaa za kimkakati za kilimo zinaweza kuliweka upya bara katika njia yake ya kulisha idadi ya watu inayoongezeka.
Hata hivyo, kama vile ambavyo ahadi za Azimio la Malabo hazikufikiwa, utekelezaji wa mipango hii unategemea utashi wa kisiasa wa nchi moja moja. Je, masaibu yanayoumiza maisha ya mamilioni ya watu barani kote yatafanikiwa kuwaamsha wanasiasa wetu wakati huu?
Johnson Kanamugire ni Mwanahabari wa majukwaa mbalimbali nchini Rwanda. Amejikita katika uandishi wa habari zinazohusiana na maisha halisi ya watu.