Ndege ya jeshi la angani nchini Kenya imeanguka katika pwani ya Kenya ya Lamu. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la nchi hiyo.
"Helikopta ya jeshi la anga la Kenya ilianguka ilipokuwa katika doria ya usiku huko Lamu Jumatatu," imesema taarifa hiyo bila kueleza iwapo kuna maafa yoyote yaliyotokea.
Lamu ni kisiwa katika bahari ya Hindi karibu na pwani ya Afrika Mashariki, takriban kilomita 241, kaskazini mashariki mwa mji wa pwani wa Kenya, Mombasa.
"Wafanyakazi na wanajeshi waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walikuwa sehemu ya kikosi cha uchunguzi wa anga cha kuimarisha doria za mchana na usiku na ufuatiliaji kwa ajili ya operesheni inayoendelea inayoitwa 'Amani Boni', taarifa hiyo ilisema.
Amani Boni ni opearesheni ya kijeshi yenye lengo la kuleta utulivu latika maeneo ya Lamu, Garissa, Tana River, Kilifi zinazopakana na msitu mpana wa Boni kuelekea mpaka wa Kenya na Somalia.
" Tunatoa rambirambi zetu kwa familia na marafiki kwa msiba mzito wa mashujaa wetu kwenye ajali ya helikopta ya Lamu," Rais William Ruto amesema katika mtandao wake wa X.
"Tunaheshimu ushujaa wao katika kutetea na kulinda uhuru wa Kenya. Sala zetu ziko kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya na wale wote ambao wameathiriwa na mkasa huo," rais Ruto ameongezea.
Wanamgambo wa al-Shabaab wamekuwa wakiripotiwa kujificha katika msitu huu na kufanya mashambulizi Kenya.
Jeshi la taifa la kenya , KDF limesema limeanzisha bodi ya uchunguzi katika eneo la tukio ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Hii sio mara ya kwanza kwa ndege ya kijeshi kuanguka nchini Kenya, ingawa taarifa kamili huwa haziwekwi wazi kutokana na unyeti wa taarifa hizo.