Kupitia mwaliko wa Rais Abdel-Fattah El-Sisi wa Misri, viongozi hao wakiwemo Rais Idriss Déby wa Chad, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Isaias Afwerki wa Eritrea, Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia, na Rais wa Baraza la Urais la Libya Mohamed al-Menfi walijadiliana kumaliza mgogoro wa Sudan ulioingia mwezi wa tatu.
Ingawa walieleza kuhuzunishwa na kuzorota kwa hali ya usalama na ubinadamu kufuatia makabiliano ya kijeshi yaliyosababisha maafa ya watu wasio na hatia na uharibifu wa mali.
Wakuu hao wametaka kukomeshwa kwa uingiliaji wowote wa nje katika mgogoro huo wakisema kuwa mzozo unaoendelea ni suala la ndani la Sudan.
Rais Abdel-Fattah El-Sisi
Viongozi hao wameshauri kufanikishwa kwa mazungumzo ya kitaifa na ya kina yenye kujumuisha wahusika wote wa Sudan, kwa kutanguliza matakwa na ustawi wa raia wa taifa hilo kwani suluhu la kisiasa linahitajika kukomesha mzozo unashuhudiwa.
Aidha, wakuu hao wamezitaka pande zote husika za Sudan kutoa ulinzi wa kutosha kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na watoaji huduma mbalimbali za kibanadamu ili kurahisisha utoaji wao misaada kwa wale wanaohitaji.
Vilevile, viongozi hao wamekubaliana kufanikisha kuwasili kwa misaada ya kibinadamu inayotolewa kwa Sudan kupitia mataifa yao, kwa uratibu na mashirika ya kimataifa yanayohusika, na kuhimiza kufunguliwa kwa njia salama kwa ajili ya kufikisha misaada kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi.
Mkutano huo wa wakuu sasa utafuatwa na mkutano wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi jirani za Sudan utakaofanyika N'Djamena Chad, ili kuratibu juhudi za pamoja za kutatua mzozo uliopo sambamba na taratibu zilizopo, zikiwemo IGAD na AU.
Katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit, na mwenyekiti wa AU, Moussa Faki Mahamat pia walihudhuria mkutano huo.