Ripoti ya UNHCR inaonyesha kuwa hadi mwisho wa 2024 mzozo huo umesababisha zaidi ya watu milioni 7 kuhama makwao ndani ya nchi / Photo: AFP

Mapigano yanayoendelea kati ya serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC na makundi yenye silaha yasiyo ya serikali yanaendelea kwa karibu miongo miwili sasa hasa katika Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR katika mtazamo wake wa 2025 linasema mzozo huo wa muda mrefu umesababisha "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na matukio mabaya ya unyanyasaji wa kijinsia."

Ripoti ya UNHCR inaonyesha kuwa hadi mwisho wa 2024 mzozo huo umesababisha zaidi ya watu milioni 7 kuhama makwao ndani ya nchi na kuwalazimu zaidi ya milioni 1 kutafuta hifadhi nje ya mipaka ya nchi.

Idadi kubwa ya raia wakiwemo wanawake na watoto wameuawa na waasi wa M23 mashariki mwa DRC,  kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa/ Picha: AFP

Nchi jirani ya Angola, Burundi, Jamhuri ya Congo, Malawi, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Tanzania na Zambia ni mwenyeji wa wakimbizi kutoka DRC.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limeendelea "kuelezea wasiwasi wake kwamba M23, Allied Democratic Forces, ADF, Democratic Force for the liberation for Rwanda (FDLR) wamezidisha ukosefu wa usalama na mateso ya raia Mashariki mwa DRC."

Makundi mengine yenye silaha ambayo Umoja wa Mataifa umebaini kuwa yanasababisha ukosefu wa usalama ni pamoja na CODECO, Zaïre Mai-Mai-Mai Kata Katanga na Malaika.

"Bado ni mara kwa mara, ramani ya vurugu inalingana na ile ya maliasili," Bintou Keita, ambaye pia anaongoza Misheni ya Umoja wa Mataifa ya Kuleta Utulivu nchini DRC, MONUSCO, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Maelfu wamelazimika kuhama makwao kwa sababu ya vita kaskazini mwa DRC/ Picha: Wengine 

Keita alibainisha kuwa M23 walichukua udhibiti wa eneo la dhahabu huko Lubera, Kivu Kaskazini, baada ya kufanya mashambulizi kuelekea Pinga mwishoni ma Oktoba 2024.

"Kulikuwa na ongezeko la 84% la kaya zilizohamishwa mwezi Novemba ikilinganishwa na mwezi uliopita, na kaya 115,084 zilizokimbia makazi katika majimbo matano ya mashariki mwa DRC," Shirika la Kibinadamu la Mercy Cops linasema katika uchambuzi wake wa kila mwezi wa hali nchini DRC.

DRC imeilaumu Rwanda kwa kuunga mkono makundi yenye silaha ya M23, huku Rwanda ikiendelea kukanusha tuhuma hizo. Kwa upande wake imeilaumu DRC kwa kuunga mkono kundi la FDLR, ambalo linapinga serikali ya Rwanda na ambalo lina kambi nchini DRC.

Rais Paul Kagame amekana tuhuma za kuunga mkono kikundi cha M23 huku akiilamu DRC kwa kuunga mkono kikundi chenye silaha cha FDLR / Picha: Reuters 

Rwanda hata hivyo, imekiri kuwa na wanajeshi na mifumo ya makombora mashariki mwa DRC kwa lengo la kulinda usalama wake, ikielekeza kwenye mkusanyiko wa vikosi vya Congo karibu na mpaka.

Juhudi za kupatanishwa kwa nchi hizo mbili ziligonga mwamba baada ya Rais wa Rwanda kushindwa kuhudhuria mkutano wa pande tatu mjini Luanda, Angola tarehe 15 Disemba, ambapo viongozi hao wawili walitarajiwa kupata muafaka wa kidiplomasia.

Mpatanishi wa Umoja wa Afrika, Rais wa Angola Joao Lourenco, alikutana na Rais wa DRC Felix Tshisekedi pekee.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi ameishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kikundi cha M23 / Picha : Getty 

"Katika mkutano wa mawaziri huko Luanda tarehe 14 Disemba hakuna muafaka uliofikiwa kati ya Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo juu ya kujitolea kwa mazungumzo ya moja kwa moja na waasi wa Congo wa M23 kwa suluhisho la kisiasa la mzozo wa Mashariki mwa DRC," Rwanda ilisema.

Ukosefu wa suluhu ya kukomesha makundi yenye silaha nchini DRC unaendelea kuweka kuhatarisha maisha na mali za raia.

Uharibifu unaosababishwa na migogoro ya Sudan na DRC ni suala linalotia wasiwasi mkubwa kwa Afrika mwaka 2025.

TRT Afrika