Wanasheria wanaomwakilisha mwanasiasa mkongwe wa Uganda Dkt. Kiiza Besigye wamekataa uamuzi wa mahakama ya jeshi nchini Uganda wa kubadilisha mashtaka dhidi ya Besigye na msaidizi wake Obeid Lutale.
Besigye ameshtakiwa na Lutale kwa makosa yanayohusiana na usalama na umiliki wa silaha kinyume cha sheria.
Wawili hao wamefikishwa tena mbele ya Mahakama ya Jeshi ya Makindye, mjini Kampala.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Kanali Raphael Mugisha, umewasilisha maombi ya kubadilisha hati ya mashtaka inayomkabili Dk. Kizza Besigye na Hajji Obeid Lutale, wakitaka kuongeza kosa jipya la uhaini.
Pia wametaka kumuweka Kapteni Denis Ola kama mshtakiwa wa ziada.
Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Martha Karua, umepinga hatua hiyo, ikitolea mfano hukumu inayosubiriwa kuhusu mamlaka ya Mahakama Kuu ya Jeshi kusikiliza kesi za raia, jambo ambalo wamelipinga.
Mawakili wa Besigye wametaka kesi hiyo kusikilizwa katika mahakama ya raia kwani Besigye si mwanajeshi tena.
Erias Lukwago ambaye ni miongoni mwa mawakili wa Dkt. Kizza Besigye, alilalamikia mahakama kuwa majina ya wale walioteuliwa kusikiliza kesi hiyo yamekuwa yakibadilika mara kwa mara tangu kuanza.
Mahakama hiyo imehoji umuhimu wa kumuachilia huru wakili mmoja wa Kiiza Besigye anayeitwa Erdona Kiiza, ambae amefungwa kwa muda wa miezi minane kwa kukiuka sheria za mahakama.
Jaji wa Mahakama ya Jeshi Brigedia Jenerali Richard Tukacungurwa ameuliza kuna haja gani ya kumuachilia wakili huyo ilhali Besigye na mwenzake tayari wana mawakili wengine 30.
Mawakili wa Besigye wanaongozwa na wakili mwandamizi kutoka Kenya Martha Karua.