Muswada wa kuongeza muda wa rais na viongozi wote waliochaguliwa kutoka miaka mitano hadi saba umechapishwa / Picha: Ikulu Kenya

Muswada wa kuongeza muda wa rais na viongozi wote waliochaguliwa kutoka miaka mitano hadi saba umechapishwa.

Muswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2024, unaofadhiliwa na Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei, sasa unatazamiwa kuwasilishwa katika Seneti kwa usomaji wa kwanza.

Sheria inayopendekezwa inaongeza muda wa kuhudumu kwa Rais, wabunge, wanachama wa bunge la kaunti yaani MCA na magavana hadi miaka saba.

Kwa sasa viongozi wanahudumu kwa miaka mitano tu, halafu uchaguzi unafanyika.

"Muswada unapendekeza kufanyia marekebisho Kifungu cha 136 cha Katiba, ambacho kinaruhusu kuchaguliwa kwa Rais, ili kuongeza muda wa Rais kutoka miaka mitano hadi miaka saba," Muswada huo unasema.

Zaidi ya hayo, Muswada huo unarekebisha Vifungu 101, 177 na 180 vya Katiba ili kuongeza muda wa wabunge, maseneta, MCAs na magavana hadi miaka saba.

Mnamo Novemba 2022, mbunge wa chama cha Rais William Ruto cha UDA alianzisha mjadala wa kuondoa ukomo wa muhula wa urais.

Mbunge wa Fafi Salah Yakub alipendekeza kuondolewa kwa ukomo wa muda na badala yake akapendekeza ukomo wa umri wa miaka 75.

Hata hivyo, pendekezo hilo lilipuuzwa.

Kwa sasa, Katiba inaweka ukomo wa mihula isiyozidi miwili ya miaka mitano mitano kwa Rais.

TRT Afrika