Rais wa Uganda Yoweri Museveni amelaani vikali uvamizi wa kigaidi uliosababisha mauaji ya watu watatu wakiwemo watalii wawili wa kigeni na raia mmoja wa Uganda Katika Hifadhi ya Kitaifa ya Malkia Elizabeth siku ya Jumanne.
"Jana, tarehe 17 Oktoba, 2023, tulikuwa na tukio la bahati mbaya na la kukasirisha katika Hifadhi ya Taifa ya Malkia Elizabeth. Watalii kadhaa pamoja na dereva wa Uganda waliuawa takriban saa kumi na mbili jioni kwenye barabara ya Katwe - Kabatooro, na kundi dogo la magaidi waliokimbia shughuli zetu nchini Kongo," Museveni alisema.
Wakati huo huo, Museveni amefichua kuwa wavamizi hao walitumia pengo la usalama lililotokana na hatua ya watalii hao kufika na kuondoka wenyewe bila walinzi wa kawaida wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda, wanao hakikisha usalama wa watalii pindi wanapozuru Hifadhi hiyo kila mara.
Museveni amelaani mauaji hayo akisema kuwa ni "kitendo cha woga cha magaidi kwa kuwashambulia raia wasio na hatia na cha kusikitisha kwa wenzi hao ambao walikuwa wameoana hivi karibuni na kutembelea Uganda kwa ajili ya fungate yao."
Katika ujumbe kupitia mtandao wa X, rais Museveni ametoa rambirambi zake kwa familia za waathiriwa huku akiahidi kuwa wahusika hao wanaoshukiwa kuwa waasi wa ADF ambao walihusika kwenye uvamizi huo, wanafuatiliwa na vikosi vya ulinzi vya Uganda.
"Ubalozi wetu wa Uganda ulioko nchini Uingereza, utafikia familia za waathiriwa na kutoa msaada wowote unaohitajika kufuatia tukio hili mbaya," Museveni alisema.