Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kurekebisha mifumo ya mashirika ya serikali kunamaanisha kuondoa uzembe / Picha: Serikali ya Uganda X. 

Mamlaka ya Maendeleo ya Kahawa ya Uganda (UCDA) ni wakala wa serikali iliyopewa jukumu la kusimamia, kukuza na kusimamia ubora wa kahawa katika mfumo mzima wa thamani. Pia ina jukumu la kusaidia utafiti na maendeleo, kukuza uzalishaji, na kuboresha uuzaji wa kahawa ili kuongeza fedha za kigeni na pia mapato ya nchi na malipo kwa wakulima.

Rais Museveni ameunga mkono hoja ya kuiondoa UCDA.

"Baadhi ya mashirika yaliundwa wakati uchumi wetu ulipokuwa unasuasua na mishahara kwa watumishi wa umma ilikuwa chini. Leo hii, baadhi ya mashirika haya yamebakia kutofanya kazi na hayana mantiki. Lengo ni kurahisisha majukumu yao kwa ajili ya utumishi wa umma wenye ufanisi zaidi, " Rais Museveni amesema katika taarifa mtandaoni.

Oktoba 24 na 25, 2024 wabunge walijipata katika majadiliano makali kati ya wale wanaotoka mikoa inayolima kahawa na wanaotoka maeneo ambayo zao hilo halilimwi.

Katika kura ya mgawanyiko, wabunge 159 waliunga mkono kupeleka Muswada kwa Kamati ya Bunge zima ili kuzingatiwa kifungu baada ya kifungu, wakati wabunge 77, kimsingi kutoka kwa upinzani, walipiga kura dhidi yake.

" UCDA inateka nyara jukumu la serikali la kutoza ushuru na kukusanya kile wanachokiita 'cess.' Mwanzoni mwa utawala wetu tulifuta ushuru wa mauzo ya kahawa nje ya nchi. Kwa nini? Ni kwa sababu haileti maana kutoza bidhaa zako za nje, sasa UCDA imerudisha hili, hapo labda ndipo sumu ipo," Rais Museveni ameongezea.

Mbali na kahawa kumekuwa na hoja ya kupunguza mamlaka zingine tofauti na kuziweka chini ya wizara husika.

"Kwa heri bodi za mamlaka, wasimamizi wakuu, makatibu binafsi, na umati wote. Baada ya kusoma kwa uangalifu, tunaweza kuchukua wakala mmoja kwa usalama na ubora wa vitu vyote vinavyoweza kumeza - vyakula na dawa - au kutenganisha chakula na dawa," Rais Museveni ameongezea.

Rais Museveni amesema kurekebisha mifumo ya mashirika ya serikali kunamaanisha kuondoa uzembe akidai ni lazima vitendo vya ubadhirifu viondolowe katika mchakato wa uzalishaji ili kuongeza maendeleo na kupunguza gharama.

"Kwa hiyo, tuliamua kufanyia kazi mashirika hayo yote yasiyo ya kutengeneza fedha. Yatakayobakia ni makampuni ya Serikali ya kutengeneza fedha - kama vile Uganda National Electricity Company Limited, Shirika la Nyumba la Taifa, NEC, UDC, nk. kufanya biashara kwa niaba ya wamiliki wa mbali na watu wa Uganda kupitia Serikali yao," Rais amesema.

TRT Afrika