Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda na sasa kiongozi wa jeshi la taifa, UPDF, amechukua rasmi hatamu ya uongozi ya jeshi.
Amechukua cheo hicho kutoka kwa jenerali Wilson Mbadi ambaye ameteuliwa na rais kuwa Waziri wa Biashara. Mbadi alikuwa kiongozi wa jeshi kwa miezi 33.
"UPDF inaendelea kuwa nguzo kuu ya amani ya Uganda ambayo wananchi wote wanaiheshimu. UPDF ni taasisi kuu ya Taifa la Uganda kwa sababu kuingia humo ni wazi kwa wananchi wote wa Uganda," Jenerali Muhoozi alisema.
Miongoni mwa majukumu ambayo kiongozi huyo mpya wa jeshi ataanza nayo ni pamoja na kuendelea kupambana na waasi wa ADF mashariki mwa DR Congo chini ya Operesheni Shuuja.
Pia ana jukumu la kupambana na wizi wa ng'ombe katika kanda ndogo ya Karamoja, na ugaidi wa mtandao miongoni mwa mengine.
Sherehe ya Muhoozi kuchukua hatamu ilifanyika katika makao makuu ya kitengo cha nne, mjini Gulu kaskazini mwa nchi.
Iliongozwa na mshauri wa rais wa masuala ya usalama Jenerali Calb Anadwanabo, maarufu kama Salim Saleh ambae ni yake Rais Museveni.
Jenerali Muhoozi sasa ni kiongozi wa 13 wa jeshi la taifa.
Amesema kuwa wananchi wa Uganda wanaweza kutofautiana kuhusu chochote lakini lazima waheshimu na kuunga mkono jitihada za jeshi la UPDF.