Hebert Hoover, aliyekuwa rais wa 31 wa Marekani kati ya 1929 na 1933, aliwahi kusema: “Watoto ndio rasilimali yenye thamani zaidi ulimwenguni.” Na Afrika imebarikiwa na rasilimali hii kwa wingi.
Idadi ya watoto chini ya umri wa miaka 18 inakadiriwa kuwa zaidi ya milioni 650, ambayo ni karibu nusu ya idadi ya watu bilioni 1.4 barani.
Kila mwaka, tarehe 16 Juni Dunia inasherehekea mtoto wa Kiafrika ambaye anashinda changamoto kadhaa - za kihistoria, kitamaduni, kiuchumi na kisiasa - ili kupata heshima na sauti katika jukwaa la kimataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, mafanikio makubwa yamerekodiwa katika upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kiafrika, huku idadi ya waliosajiliwa kujiunga elimu ya msingi Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiongezeka hadi 79% katika 2018, kutoka 60% mwaka 2000.
Maendeleo katika elimu yanafanywa kutokana na serikali kukumbatia elimu ya msingi na kuanzisha sera zinazopendelea elimu shuleni, Dk. Joan Nyanyuki, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Sera ya Mtoto wa Afrika, anaiambia TRT Afrika.
“Kuna watoto wengi baŕani Afŕika ambao sasa wanapata elimu ya msingi bila malipo. Nchini Zambia, kwa mfano, kuna programu ya bure ya elimu ya msingi na sekondari. Katika nchi nyingine nyingi za Afrika, elimu ya msingi imekuwa ya lazima,” anasema Dk. Nyanyuki.
Anasema ujumbe uliotumwa wakati wa mapambano ya mataifa ya Kiafrika ya kujitawala - kwamba elimu pekee ndiyo ingeweza kuliondoa bara hilo na watu wake kutoka umaskini - ulisaidia kuleta mabadiliko makubwa katika mtazamo wa elimu kwa waafrika.
Enzi ya kidijitali
Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika mwaka huu ni 'Haki za Mtoto katika Mazingira ya Kidijitali.'
Upatikanaji wa mtandao wa nyumbani miongoni mwa watoto barani Afrika, hata hivyo, bado ni mdogo, huku 13% pekee ya watoto katika Mashariki na Kusini mwa Afrika wanapata intaneti.
Afrika Magharibi na Kati, idadi hiyo ni chini ya 5% , ripoti ya UNICEF inaonyesha. Katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ni asilimia 25 tu ya vijana wanapata intaneti nyumbani.
Dk. Nyanyuki anasema kuna muunganisho wa intaneti wa kutumiw ana watoto ni msumeno unaokata ande mbili.
"Kwa upande mmoja, imeboresha upatikanaji wa taarifa, kuwezesha mawasiliano, kurahisisha upatikanaji wa nyenzo za kujifunzia, kumfungua macho mtoto wa Kiafrika kwa ulimwengu, na kuwezesha kujifunza kwa mbali," anasema.
"Kwa upande mwingine, imewaweka watoto kwenye hatari ya unyanyasaji na kutumiwa vibaya ikiwa ni pamoja na kutumiwa kingono, picha za kutisha, na uonevu," Dk. Nyanyuki anaongeza.
Wataalamu wanasema kuna haja ya kuhamasisha watoto - hasa wale kutoka Afrika - kuhusu haki zao za kidijitali, na pia kuja na sera zinazowalinda dhidi ya unyonyaji kwenye mifumo ya kidijitali.
Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mazingira ya kidijitali linasema kila serikali ina wajibu wa kukuza, kuheshimu, kulinda na kutimiza haki zote za watoto katika mazingira ya kidijitali.
Kuwalinda watoto
Haki za mtoto katika mazingira ya mtandaoni ni pamoja na kutobaguliwa, maslahi bora, haki ya kuishi, kukua pamoja na kuheshimu maoni ya mtoto.
"Mtoto wa Kiafrika ana changamoto za kipekee, linapokuja suala la ufikiaji sawa na wa mazingira ya kidijitali. Tofauti na watoto kutoka mabara mengine, nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na uhaba wa umeme, machafuko ya kisiasa na ukosefu wa mtandao," anasema Dk. Nyanyuki.
Mataifa ya Kiafrika, hata hivyo, yamepiga hatua za kupongezwa katika kuhakikisha kwamba watoto wanaopata vifaa vya kidijitali wanalindwa dhidi ya madhara. Ingawa, kazi zaidi bado inahitaji kufanywa, tafiti zinaonyesha.
Kwa mfano, 2019 Kenya ilipitisha sheria iliyosema kwamba taarifa za kibinafsi kuhusu watoto haziwezi kusambazwa bila idhini ya mzazi au mlezi wa mtoto na kwa njia ambayo inalinda hadhi yake na kuendeleza haki na maslahi ya mtoto.
Afrika Kusini inalinda kwa nguvu haki za watoto katika anga ya kidijitali, huku Ghana ilipitisha Sheria ya ulinzi wa data 2012 ili kuwakinga watoto dhidi ya unyanyasaji mtandaoni.
Takriban nchi 32 za Afrika zimetunga sheria za ulinzi wa data, lakini sio zote zinazolinda watoto kwa njia dhahiri.
Ajenda ya Umoja wa Afrika (AU) kwa ajili ya Watoto 2040, ambayo inalenga kukuza Afrika yenye kutoa kipaumbele kwa haki za mtoto, inaziomba nchi wanachama kuwapa watoto vifaa vya bei nafuu vya teknolojia ya habari na mawasiliano, maudhui, na muunganisho, pamoja na kujumuisha vipengele hivi katika mitaala ya elimu.
Programu za utaftaji
Florence Ogonjo na Rachel Achieng wa Chuo Kikuu cha Strathmore nchini Kenya wanasema katika utafiti wao kwamba watoto, wazazi na walimu wanahitaji kuhamasishwa kuhusu usalama wa mtandaoni na matumizi ya watoto kuwajibika katik autumiaji wa kompiuta.
Maxim Murungweni, mratibu wa mradi wa Child Helpline International katika Mashariki na Kusini mwa Afrika, anaiambia TRT Afrika kwamba taarifa zozote mbaya zinazosambazwa mtandaoni kuhusu watoto zinaweza kuwaathiri maisha yao yote kwa sababu "binadamu husahau, lakini mtandao hausahau" .
Kichochezi cha lugha
Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika ina mizizi yake katika tukio la bahati mbaya lililotokea Juni 16, 1976 huko Soweto, Afrika Kusini.
Siku hiyo, wanafunzi wapatao 20,000 waliingia katika mitaa ya Soweto wakidai kufundishwa kwa lugha wanayoielewa.
Maafisa wa polisi wa utawala wa kibaguzi wakati huo walijibu kwa kuwaua mamia ya waandamanaji. Serikali ya Afrika Kusini - baada ya kupata uhuru - ilitenga Juni 16 ya kila mwaka kama sikukuu kuadhimisha tukio hilo.
Tarehe hiyo baadaye ilitambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika baada ya Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) kukubali kuadhimisha mtoto wa Afrika Juni 16 kila mwaka.
Mara ya kwanza kwa siku hii kuadhimishwa kimataifa ni Juni, 1991. Siku hiyo inaangazia vikwazo ambavyo watoto wa Kiafrika wanakabiliwa navyo ili kupata elimu bora pamoja na kuangazia hatua zilizopigwa.
Prof. Enos Ngutshane, mkurugenzi wa taasisi inayosimamia hazina ya malipo ya uzeeni Afrika, alikuwa miongoni mwa vijana walioandamana kupinga kulazimishwa kwa lugha nchini Afrika Kusini mnamo 1976.
"Nilikamatwa siku mbili kabla ya Juni 16 kwa kumwandikia barua ya kupinga waziri wa wakati huo wa Apartheid baada ya kujua kwamba taasisi hiyo ilikuwa na mpango wa kubadilisha lugha shuleni," Ngutshane anaiambia TRT Afrika.
Anasema wakoloni wenye asili ya Uholanzi walitaka kuanzisha lugha ya Kiafrikana kuchukua nafasi ya Kiingereza shuleni.
Alisema alishtakiwa kwa 'uchochezi' mnamo Juni 16, lakini serikali ilitupilia mbali kesi yake kufuatia shutuma zilizotokea kufuatia mauaji yaliyofanywa kuzima maandamano.
“Maafisa wa polisi walikuwa wakiwapiga risasi watoto kiholela. Majirani zangu kadhaa walipoteza wapendwa wao kwa kupigwa risasi,” alisema Ngutshane.
Kipaumbele kwa elimu
Watoto milioni 98 Kusini mwa Jangwa la Sahara kati ya umri wa miaka sita na 18 bado hawako shuleni, UNESCO ilisema katika ripoti ya 2022.
Bara la Afrika, hata hivyo, limeweza kuondoa pengo la jinsia katika upatikanaji wa elimu, huku idadi ya wanafunzi wa kike ikiwa sawa na ya wanafunzi wa kiume.
Kwa mujibu wa shirika la UNESCO, idadi ya watoto ambao walikuwa nje ya shule kufikia 2022 ilikuwa kubwa zaidi nchini Nigeria (milioni 20.2), ikifuatiwa na Ethiopia (milioni 10.5) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (milioni 5.9).
Morocco, Misri, Zambia, Kenya, Tanzania, Zimbabwe, Malawi, Burundi na Lesotho ni baadhi ya nchi za Afrika zinazotoa elimu bila malipo katika shule za msingi za umma.
Wakati Tanzania inaanzisha mpango wa elimu bure ya msingi na sekondari mwaka 2014, kulionekana kupungua kwa idadi ya watoto wa mitaani, japo inaaminiwa kuwa watoto wengi zaidi wako mitaani kwa sababu ya umaskini.
Utegemezi wa watoto
Changamoto nyingine kubwa inazomkabili mtoto wa Kiafrika hivi leo ni uhaba wa huduma za afya, ajira kwa watoto, utapiamlo, unyanyasaji wa kingono, dhuluma za nyumbani, migogoro na ukosefu wa makazi.
"Serikali za Afrika zinapaswa kuhakikisha zinaelekeza sehemu kubwa ya bajeti zao kwa ustawi wa watoto. Kuna ushahidi unaopendekeza nchi zinazowekeza kwa kiasi kikubwa kwa watoto zinafanya vyema zaidi kiuchumi, kwa sababu zinawekeza kwenye rasilimali sahihi kwa siku zijazo,” anasema Dk. Nyanyuki.
Prof. Ngutshane, kwa upande wake, alirejea nukuu maarufu ya Rais Herbert Hoover kuhusu watoto kuwa rasilimali ya thamani zaidi duniani.
"Wito wangu kwa mtoto wa Kiafrika ni kwamba, tafadhali jielimishe kama darasa la [Afrika Kusini] la 1976 kwa sababu tunakutegemea kama viongozi wetu wa baadaye. Bara hili lote lazima liendeshwe na wewe."