Ummy Mwalimu

Kifo cha mtoto huyo kimefikisha idadi ya wagonjwa kuwa sita waliokufa kutokana na ugonjwa huo tangu ulipolipuka mkoani humo Machi 21, 2023. Taarifa hiyo ilitangazwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipotoa taarifa ya ugonjwa huo.

Katika maongezi na TRT Afrika leo asubuhi, Diwani wa kata ya Kanayangereko, wilaya ya Bukoba, Hamisi Hassan Byeyombo, ambapo ugonjwa ulipotambulika kwa mara ya kwanza, alithibitisha hizo habari na kuongeza kuwa "mtoto alifariki wiki mbili zilizopita" ila hawakutangaza.

Byeyombo amesema "mtoto huyo na mama yake waligundulika kuwa na ugonjwa huo na alikuwa akitibiwa katika kituo cha kutengwa karantini."

Diwani Byeyombo ndiye alikuwa wa kwanza kutoa taarifa kwa Wizara ya Afya kwamba ugonjwa wa ajabu umekuwa ukiwaua watu kijini kwake na ukagundulika badae kwamba ugonjwa ni Marburg.

Kupitia taarifa kwa umma, Waziri Mwalimu aliongeza kuwa tangu kuzuka kwa ugonjwa huo Machi 21, wagonjwa tisa wameripotiwa ambapo wagonjwa watatu walipona na sita akiwemo mtoto huyo na mhudumu wa afya walifariki.

Alisema watu 211 kati ya 212 waliowekwa karantini waliachiwa baada ya kufuatiliwa kwa siku 21 na kubainika kuwa hawakuathiriwa na ugonjwa huo.

Aliongeza kuwa serikali ilikuwa ikizingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani, WHO, juu ya ufuatiliaji wa magonjwa ya milipuko, ikiwa pamoja na MVD.

Alisema serikali itatangaza udhibiti kamili wa ugonjwa huo baada ya siku 42 tangu mgonjwa wa mwisho anayeshukiwa kugunduliwa kuwa hana maambukizi au ugonjwa - kama mwongozo wa WHO, na kusema kuwa tarehe itakuwa Mei 31, 2023.

Aliwataka wahudumu wa afya Afrika Mashariki kuzingatia miongozo ya kuzuia na kudhibiti maambukizi.

TRT Afrika