Niger na Nigeria ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa mtama. Picha: FAO

Mnamo mwezi Machi 2021, kikao cha 75 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kiliamua kutangaza 2023 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Mtama.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) liliorodhesha "sababu sita za kupeleka mtama sokoni".

Afrika ni kama uwanja mgumu unaoweza kupima ufanisi wa kitu chochote. Hivyo Afrika inaweza kuongeza sababu nyingine ya saba ili kuishawishi dunia kukumbatia mojawapo ya vyakula vinavyoonekana ni duni.

Utetezi wa FAO kwa mtama unalifanya zao hili lenye mbegu ndogo, linazokuzwa duniani kote kama nafaka kwa matumizi ya binadamu au malisho ya mifugo na, kuwa kileleni miongoni mwa msururu wa chakula. Hali hii inaangazia pia suala la uendelevu, maendeleo ya kiuchumi na thamani ya lishe.

Haijalishi kama inaliwa kama nafaka tu au kusindikwa kuwa unga, sifa za lishe za mtama hupita zile za nafaka nyingine kama wali mweupe.

Dk Muhammad Baba Bello, mwanauchumi wa kilimo mwenye uzoefu wa shambani huko Afrika Magharibi, anatetea matumizi ya mtama katika kupambana na utapiamlo katika jamii za Kiafrika na kuimarisha uendelevu wa kiuchumi wa kaya za vijijini.

Dkt Bello, ambaye anafanya kazi na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki nchini Nigeria, anabainisha kuwa ingawa kaya nyingi za vijijini barani Kiafrika hutumia mtama kwa njia mbalimbali, baadhi hazijui thamani halisi ya lishe yao.

Mifuko ya mtama katika moja ya soko kubwa la nafaka Afrika Magharibi, soko la Dawanau huko Kano, Nigeria. Picha: TRT Afrika

"Mtama unaweza kuimarishwa na hata kw kuongeza virutubisho vidogo vidogo na vitamini. Lakini kwanza, unahitaji kukuza mnyororo wa thamani wa mtama kwa kuwekeza katika kuongeza thamani yake sokoni ili kuendana na ile ya mahindi au soya, ambayo hutumiwa katika sekta mbalimbali, ” anaiambia TRT Afrika.

Mtama kama chakula kikuu

Kulingana na FAO, mtama ni miongozi mwa makundi tofauti cha nafaka za ardhi kavu.

Kampeni inayoendelea inaangazia faida za mtama kama chakula cha msingi kinachostahimili hali ya hewa, chenye faida za kiafya, fursa za maisha vijijini, usalama wa chakula na matumizi anuwai ya chakula na dawa.

Nafaka hizi sio tu hukua mahali ambapo zingine haziwezi, pia zinaboresha kiwango cha udongo na mfumo wa ikolojia, kulingana na wataalam.

Mbali na kuwa zao linalohimili ukame kulingana na hali ya udongo, aina yoyote ya mtama ni chanzo kizuri cha madini ya kalsiamu, manganese, fosforasi, potasiamu, shaba, nyuzinyuzi za chakula na madini.

Kama chakula, mtama ni nafaka ya asili isiyo na gluteni. Aina zinazopatikana kwa kawaida ni pamoja na mtama lulu, uwele na mtama mweupe.

Takwimu kutoka kwa FAO zinaonyesha kwamba mtama hulimwa katika bara la Asia na Afrika, huku India ikiwa mzalishaji mkuu, ikifuatiwa na Nigeria, Niger na China.

Katika Afrika Magharibi, wakulima kwa kawaida hupepeta mtama kwa mikono - Picha: Reuters

Katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, mtama ni chakula kikuu cha kitamaduni. Katika nchi za Afrika Magharibi, ikiwa ni pamoja na Nigeria na Niger, mtama hutumika kutengeneza aina mbalimbali za vyakula na vinywaji vya kienyeji kama vile Tuwo, Biski (nafaka iliyochemshwa), Waina (iliyochomwa), Kunu (gruel), Fura (mipira iliyoviringishwa) na Tumu (nafaka iliyochomwa kwenye mabua).

Nasiru Baita, mkulima wa mtama katika eneo la Jahun katika jimbo la Jigawa kaskazini-magharibi mwa Nigeria, anakumbuka kwa hisia kidogo jinsi wazazi wangewanywesha watoto wao uji uliotengenezwa kwa mtama ili kusaidia ukuaji mzuri na kinga. Baadhi ya watu hasa wa vijijini bado wanafuata lishe hii.

Kuonyesha imani yake kwa mtama, Nasiru anabakia kuwa mkulima anayezingatia lengo kubwa zaidi.

"Baada ya kuvuna mtama msimu uliopita, sasa nimesafisha shamba langu kwa maandalizi ya msimu mwengine mwaka huu. Na tayari nimeweka samadi ya ng'ombe kama mbole ya kupandia," anaiambia TRT Afrika.

Kama ilivyo kwa wakulima wengi katika eneo hili wanaojiandaa kwa msimu mpya wa kilimo kuanzia mwishoni mwa Mei au mapema Juni, Nasiru anatumai kuwa hali ya hewa itakuwa njema.

"Kimsingi, tunasubiri mvua kubwa ya kwanza msimu huu. Mtama wetu ni zao la siku 90," anasema.

Moja ya changamoto zinazowakabili wakulima barani Afrika ni mafuriko ya mara kwa mara. Picha: Reuters

Tofauti na siku za nyuma, wakulima wa mtama sasa wanapata aina bora ya mbegu kupitia ruzuku kutoka kwa wakala wa huduma za kilimo za serikali ya jimbo.

Lakini wakulima wengi katika jamii ya Nasiru bado wanatumia mbegu za asili, ambazo wanahifadhi kila baada ya mavuno.

Haja ya kuongeza thamani

Kulingana na Dk Bello, tatizo kubwa la uzalishaji wa mtama barani Afrika ni ukosefu wa uongezaji thamani wa soko. "Utafiti wa sasa unalenga zaidi aina za mbegu na ustahimilivu wa udongo, hatua ambazo hazitoshi," anasema.

Abbas Zubairu, mkulima mwingine mdogo kaskazini mwa Nigeria, anasema moja ya changamoto kuu katika ukuzaji wa mtama ni gharama kubwa ya mbolea.

Hii inawalazimu wakulima wengi kutegemea mbolea ghali zaidi inayopatikana katika masoko ya ndani.

Mwaka jana, Abbas alizalisha magunia 30 ya mtama, kila moja ikiwa na kilo 50, lakini kutumia pesa nyingi kwenye mbolea kulipunguza mafanikio yake.

"Nilinunua mfuko wa mbolea ya NPK kwa N18,000 (dola 40), baada ya kukosa mbolea ya ruzuku ya Serikali inayouzwa kwa N15,000 (dola 33). Pia nilinunua mfuko wa mbole ya urea kwa N27,000 (dola 60) sokoni, ambayo serikali inauza kwa N22,000 (dola 48)," anasema.

Baadhi ya wakulima wanasema gharama kubwa ya pembejeo huathiri faida zao katika masoko. Picha: TRT Afrika

Katika masoko ya ndani ya Jahun, bei ya mtama ilipanda msimu huu kwa zaidi ya N25,000 ($55) kwa mfuko wa kilo 50. Hii pia ndiyo bei iliyopo katika soko la Gujungu na Kafin-hausa, yote katika jimbo la Jigawa.

Dk Ayuba Ibrahim Adamu, ambaye anashiriki katika kipindi cha lishe cha kila wiki katika kituo cha redio cha eneo hilo kaskazini mwa Nigeria, anasema mtama unapaswa kupatikana kwa bei nafuu kwa kila mtu kwa sababu ya thamani yake ya lishe na matibabu.

"Ulaji wa mtama husaidia kudhibiti ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na viwango vya cholesterol. Lakini tunahitaji kuelimisha watu wetu zaidi," anasema.

"Katika orodha ya vyakula bora vya asili, hakuna kitu kinachokaribia mtama katika suala la thamani ya lishe na hali yake ya bei. Ninakula mtama kila siku, hata katika hafla maalum," anaongeza.

Dkt Bello anasisitiza umuhimu wa mtama kwa Afrika. "Mtama ulikuwa chakula kikuu Afrika hata kabla ya mchele na mahindi kuja kwetu. Pale ambapo mazao kama vile mahindi yanafeli, mtama hustawi hata kukiwa na mbolea kidogo."

Wataalam wanakubaliana kwamba kuongeza uzalishaji wa mtama kunaweza kusaidia kukabiliana na uhaba wa chakula na kuongeza mapato kwa serikali pamoja na wakulima, hasa katika nchi za Kiafrika ambazo zina nafasi nzuri zaidi ya kulima zao hili bora.

TRT Afrika