Mkutano wa siku tatu wa viongozi wa Afrika wa Mbolea na Afya ya Udongo barani Afrika umeanza jijini Nairobi, nchini Kenya. Mkutano huo utafanyika kati ya tarehe 7 had 9 Mei mwaka huu.
Viongozi wa wataalamu wa kilimo wanakutana kujadili kuhusu kupungua kwa ubora wa udongo Afrika kwa miongo kadhaa - jambo ambalo Umoja wa Afrika unasema linaendelea kuathiri vibaya uwezo wa uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula katika bara hilo.
Mnamo Juni 2006, viongozi wa Afrika waliidhinisha 'Azimio la Abuja kuhusu Mbolea' kwa ajili ya kuboresha kijani ya Afrika na kuweka mkakati wa bara wa kubadilisha mwelekeo unaotia wasiwasi wa uzalishaji duni Afrika.
Kulingana na Umoja wa Afrika , azimio hilo lililenga kuongeza ukuaji wa kilimo, usalama wa chakula, na maendeleo ya vijijini barani Afrika, kwa kuzingatia jukumu la mbolea.
Viongozi walipendekeza kuongeza matumizi ya mbolea kutoka kilo 8 kwa hekta hadi kilo 50 kwa hekta katika miaka 10.
Nchi zilizotimiza makubaliano ya Azimio hilo
Umoja wa Afrika unasema nchi ambazo zimefikia matumizi ya kilo 50 ya mbolea kwa hekta ni:
Morocco 55.29
Eswatini 57.77
Botswana 59.27
Kenya 60.66
Zambia 63.90
Malawi 96.74
Afrika Kusini 104.64
Mauritius 186.50
Ushelisheli 542.47
Misri 542.57
"Kupungua kwa afya ya udongo kumezuia ufanisi wa matumizi ya mbolea na kutatiza ukuaji wa tija ya kilimo, usalama wa chakula, na uendelevu wa mazingira katika bara zima," kamishna wa kilimo wa Tume ya Umoja wa Afrika, Josefa Sacko amesema katika mkutano huo.
"Matokeo yake, ukuaji wa uchumi na ustawi—hasa kwa wakazi wa vijijini, ambao wanapata riziki zao moja kwa moja kutokana na kilimo – katika bara hili vimetatizika. Kwa hiyo, ni wakati muafaka wa kukagua hali ya afya ya udongo barani Afrika ili kurekebisha mikakati inayowekwa kwa ajili ya kuongeza tija ya udongo," Sacko ameongezea.
Umoja wa Afrika unasema katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la matumizi ya rasilimali za madini za Kiafrika kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea. Hata hivyo, wingi wa uzalishaji huu unasafirishwa nje ya nchi.
Hii ni mojawapo ya ajenda ambayo itajadiliwa katika mkutano huu wa Nairobi.
Marais wa Afrika wanatarajiwa kufanya majadiliano tarehe 9 Mei.