Haya yamesemwa leo, Alhamisi, Agosti 1, 2024, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali na wananchi waliohudhuria ufunguzi wa Maonyesho ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi na Sherehe za Nanenane za Mwaka 2024 katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma.
"Katika sekta ya kilimo, hadi Juni, 2024, Serikali imefanikisha upatikanaji wa masoko katika nchi za China, India, Marekani, Pakistan na Brazil, ambapo tani milioni 1.574 za matunda na mazao ya jamii ya kunde yenye thamani ya dola za kimarekani trilioni 2.329 zimeuzwa katika nchi hizo," alisema.
Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imeingia mkataba wa kuuza tani milioni 1.25 za mahindi. "Kati ya hizo, tani 650,000 zitauzwa Zambia; tani 500,000 zitauzwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na tani 100,000 kwa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa."
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imefanikisha upatikanaji wa soko la vanila, pilipili manga, karafuu, nanasi, kakao, viazi mviringo, tumbaku na ndizi katika nchi za China, Marekani, Pakistan, Afrika Kusini na India, ambazo zinatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.
"Kwa upande wa wafugaji, hadi Aprili, 2024 jumla ya tani 13,745 za nyama zenye thamani ya dola milioni 56 za Marekani zimeuzwa katika nchi za Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Vietnam. Pia, vipande 1,542,916 vya ngozi vyenye thamani ya shilingi bilioni saba vimeuzwa Nigeria, Togo, Kenya, Ethiopia na Pakistan."
Kuhusu sekta ya uvuvi, Waziri Mkuu amesema kuwa hadi Aprili, 2024, jumla ya tani 41,271 za bidhaa za uvuvi na samaki hai wa mapambo 134,572, vyenye thamani ya shilingi bilioni 515.78, vimeuzwa katika nchi za Umoja wa Ulaya, Canada, Marekani, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, China, Zambia, Uganda na Malawi.
Sekta ya kilimo
Akifafanua juhudi zilizochukuliwa na Serikali kuendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, Waziri Mkuu amesema sambamba na nia na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuongeza ajira kwa vijana na wanawake kupitia mpango wa Jenga Kesho Iliobora.
"Kupitia mpango huo, vijana 686 wanaendelea na biashara ya kilimo katika mashamba ya pamoja na tayari wameanza uzalishaji. Kwa upande wa ufugaji, vijana 161 wanaendelea na mpango wa kunenepesha mifugo katika vitalu vya Mashamba ya Taifa (NARCO). Sekta ya uvuvi haikuachwa nyuma, vijana 200 tayari wamefundishwa na vijana 300 wanaendelea na mafunzo ya ufugaji wa samaki."
Awali, akimwalika Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema wizara yake imeanza kutekeleza maagizo ya Rais Hassan ya kujenga miundombinu ya kudumu katika maeneo ya kanda ambako maonyesho ya Nane Nane yanafanyika ili kuwezesha maeneo hayo kufanya kazi kwa mwaka mzima.
Alisema uwanja wa Nzuguni, unaohudumia mikoa ya Dodoma na Singida, utajengwa kwa awamu tatu hadi kukamilika kwake na utagharimu shilingi bilioni 40. "Tumeanza kujenga uzio, kutakuwa na maeneo ya shughuli za uzalishaji kwa mwaka mzima, kutakuwa na kumbi za mikutano, vituo vya kukuza vijana wanaofanya shughuli za teknolojia."
Ametaja viwanja vingine vitakavyoboreshwa kuwa ni Johh Mwakangale (Mbeya), Julius Nyerere (Morogoro), Themi (Arusha) na Ngongo (Lindi). Amesema mwakani, ujenzi wa viwanja vya Kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa utaanza.
Amesema katika kilele cha sherehe hizo Agosti 8, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua kiwanda cha kuunganisha matrekta kinachojengwa hapo Nzunguni na vifaa kwa ajili ya wakulima. Atazindua matrekta 500 ya kwanza na powertillers 800.
Amesema lengo ni kuzalisha matrekta 10,000 ifikapo mwaka 2030 ili wakulima wadogo waweze kuyakodi. "Mkulima hahitaji kununua trekta kwa shilingi milioni 60, anahitaji shamba lake lilimwe na trekta, lipandwe kwa planter, apate boom sprayer. Serikali inawekeza pesa katika eneo hilo," alisema.