Vurugu zinaendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali ya nchi hiyo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais./Picha: @TheAfrican_Wave

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi ameziomba jumuiya za kimataifa kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na vurugu baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini humo.

Siku ya Oktoba 24, 2024, Tume ya Uchaguzi ya Msumbiji ilimtangaza mgombea wa chama cha Frelimo Daniel Francisco Chapo mshindi wa Uchaguzi wa Rais uliofanyika Oktoba 9, mwaka huu.

Katika kikao na mabalozi wa nje kilichofanyika jijini Maputo, Nyusi ambaye anaondoka madarakani baada ya kuhudumu kwa kipindi cha mihula miwili, alisisitizia umuhimu wa kudumisha amani kwa maendeleo ya nchi hiyo baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa mwaka 2024.

“Tunaendelea kuwaomba wadau wetu wa kimataifa kuendelea kuiunga mkono Msumbiji, hasa katika nyakati hizi,” Rais Nyusi alisema.

“Vurugu hizo zimeleta uharibifu mkubwa,” alieleza.

Kulingana na Rais Nyusi, juhudi za kudumisha amani nchini humo ni lazima ziungwe mkono na jumuiya za kimataifa, hususani wkati nchi hiyo inapitia changamoto za kijamii na kiuchumi.

TRT Afrika