Mwanamume aliyedaiwa kumvamia mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei amefariki kutokana na majeraha aliyopata alipomwagia petroli mwanariadha huyo wa Olimpiki, hospitali ya Kenya iliyokuwa ikimtibu ilisema Jumanne.
Polisi walisema kuwa Dickson Ndiema Marangach alimvamia Cheptegei nyumbani kwake magharibi mwa Kenya mnamo Septemba 1. Mama huyo wa watoto wawili alipata asilimia 80 ya majeraha ya moto na alifariki wiki jana.
Wakati wa shambulio hilo Marangach pia alipata asilimia 30 ya majeraha ya moto na alikuwa akitibiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Moi Teaching and Referral Hospital (MTRH) katika jiji la Rift Valley Eldoret.
"Ni kweli tulimpoteza Dickson Ndiema jana usiku mwendo wa saa 8:00 usiku," afisa katika idara ya mawasiliano ya hospitali hiyo aliiambia AFP, akiomba kutotajwa jina kwa kuwa hawakuruhusiwa kuzungumza na waandishi wa habari.
Ukatili wa kijinsia
Familia yake ilikuwa imefahamishwa, afisa huyo alisema, akiongeza kuwa "taarifa kamili" itatolewa baadaye.
Shambulio dhidi ya Cheptegei mwenye umri wa miaka 33 limepokelewa kwa huzuni na hasira ikiwa ni mfano mwingine wa kutisha wa unyanyasaji wa kijinsia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Takriban wanariadha wengine wawili wamepoteza maisha mikononi mwa washirika wao tangu 2021.
Cheptegei anatarajiwa kuzikwa Septemba 14 karibu na nyumba ya familia yake mashariki mwa Uganda, kulingana na Kamati ya Olimpiki ya nchi hiyo.
Jinsi ilivyotokea
Shambulio hilo, ambalo vyombo vya habari vya nchini vilisema lilishuhudiwa na binti za Cheptegei, lilikuja wiki chache tu baada ya kucheza kwa mara ya kwanza katika mbio za marathon za wanawake katika Michezo ya Paris, ambapo alimaliza wa 44.
Polisi walisema Marangach alijificha nyumbani kwake huko Endebess, karibu na mpaka na Uganda, alipokuwa kanisani na watoto wake.
Babake, Joseph Cheptegei, aliambia wanahabari mzozo kati yake na Marangach ulikuwa kuhusu mali alikokuwa akiishi na dadake na binti zake.
Aliambia vyombo vya habari vya Kenya wiki jana kwamba Marangach alikuwa amenunua lita tano za petroli kisha akajificha kwenye banda la kuku kabla ya shambulio hilo.