Ajali hiyo katika mji wa Kigogwa, takriban kilomita 25 kaskazini mwa mji mkuu wa Uganda Kampala ilitokea Oktoba 22, 2024. / Picha: Reuters

Idadi ya vifo kufuatia mlipuko wa lori la mafuta karibu na mji mkuu wa Uganda Kampala wiki iliyopita imeongezeka hadi 24, serikali ilisema Jumapili.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki imeshuhudia maafa kadhaa kama hayo katika miaka ya hivi karibuni, huku watu wakikimbilia kuiba mafuta kutoka kwa malori ya kusafirisha mafuta yaliyohusika katika ajali za barabarani.

"Ajali mbaya" iliyotokea Jumanne katika mji wa Kigogwa, takriban kilomita 25 (maili 15) kaskazini mwa Kampala, ilisababisha "11 walioripotiwa kufariki katika eneo la tukio", alisema Waziri wa Mawasiliano Godfrey Kabbyanga katika taarifa yake.

Aliongeza kuwa "wengine 13 wamefariki tangu wakati huo katika hospitali ya Kiruddu na hospitali ya kijeshi ya Bombo na kufanya idadi hiyo kufikia 24."

Utambulisho wa maiti

“Tangu baadhi ya waliofariki kuteketea kiasi cha kutotambulika, polisi wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuwabaini marehemu kwa kupima DNA,” alisema.

Lori hilo lilikuwa limeondoka katika mji mkuu kuelekea Gulu kaskazini mwa Uganda, safari ya takriban kilomita 650 (maili 403), lakini lilipinduka na kuwaka moto ikiwa njiani.

Dereva huyo bado hajulikani aliko, kwa mujibu wa serikali.

Watu kadhaa wamesalia hospitalini, kulingana na shirika la utangazaji la NTV.

Matukio mengine

Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya lori la mafuta kulipuka kaskazini mwa Nigeria mnamo Oktoba 15 na kuua zaidi ya watu 170.

Mnamo Agosti 2019, watu kumi na tisa walikufa wakati lori la mafuta lilipogonga magari mengine katika mji wenye shughuli nyingi wa Kyambura magharibi mwa Uganda na kulipuka.

Mnamo 2002, watu sabini waliuawa wakati lori la mafuta lilipogonga basi huko Rutoto, chini ya kilomita 50 kutoka Kyambura.

Na mwaka 2013, watu 33 walifariki katika mlipuko baada ya lori la mafuta kupinduka mjini Kampala.

Lori mbili za mafuta zagongana

Siku ya Jumamosi, lori mbili za mafuta zilipinduka kwenye barabara inayounganisha Uganda na Rwanda - moja likiwa limegongana na lori la mizigo, na kusababisha kifo cha dereva na msaidizi wake, na nyingine kushika moto bila kusababisha maafa.

TRT Afrika