Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasili Mogadishu, mji mkuu wa Somalia siku ya Jumanne mwanzoni mwa ziara fupi kwenye nchi hiyo iliyokumbwa na vita na majanga ya hali ya hewa.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha Guterres akilakiwa katika uwanja wa ndege katika mji mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Abshir Omar Huruse.

Anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo kuhusu masuala yanayo husu ukosefu wa usalama, athari za mabadiliko ya hali ya hewa na mwitikio wa kibinadamu nchini humo.

Hii ni sehemu ya ziara za mkuu wa Umoja wa Mataifa za mshikamano wa Ramadhani katika nchi zilizochaguliwa zenye Waislamu wengi kila mwaka.

Mapema wikihii Bw Guterres alisema kupitia mtandao wa twitter ''kwangu mimi, ziara zangu za jadi za mshikamano wa Ramadhani ni fursa ya kukumbuka umuhimu wa kuleta amani duniani. Fursa ya kutiwa moyo.''

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia alitoa wito wa umoja kati ya jumuiya mbalimbali za kidini akisema ''sote tuje pamoja katika mshikamano, bila kutegemea imani zetu za kidini.''

Somalia imeweka kizuizi cha usalama Mogadishu kwa ziara hiyo ambayo haijatangazwa, huku barabara nyingi zikiwa zimefungwa, na usafiri wa umma umezuiliwa.

Kuwasili kwa Guterres kunakuja wakati nchi hiyo inakabiliwa na ukame mbaya ambao umewapeleka wengi kwenye ukingo wa njaa, huku serikali pia ikishiriki katika mashambulizi makubwa ya kukomesha uasi wa umwagaji damu unaoendeshwa na kundi la al Shabaab.

Umoja wa Mataifa umezindua ombi la dola bilioni 2.6 kwa ajili ya msaada wa kibinadamu kwa taifa hilo lenye matatizo la Pembe ya Afrika, lakini kwa sasa linafadhiliwa kwa asilimia 13 pekee.

Misimu mitano ya mvua iliyoshindwa mfululizo katika baadhi ya maeneo ya Somalia pamoja na Kenya na Ethiopia imesababisha ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo minne, na kuangamiza mifugo na mazao na kuwalazimu watu wasiopungua milioni 1.7 kutoka makwao kutafuta chakula na maji.

Wakati vizingiti vya njaa havijafikiwa nchini Somalia, Umoja wa Mataifa unasema takriban nusu ya wakazi wake watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu, huku milioni 8.3 wakiathiriwa na ukame.

Antonio Guterres alianza utamaduni wake wa kufanya ziara ya mshikamano wakati wa Ramadhani, alipokuwa Kamishna Mkuu wa Wakimbizi, akiendesha shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR - kazi aliyoifanya kwa miaka kumi, kabla ya kuchukua kazi kuu ya Umoja wa Mataifa mwaka 2017.

Mwaka jana alizuru Nigeria, Niger na Senegal ambako alizungumzia masuala ya ukosefu wa usalama, mabadiliko ya hali ya hewa na athari za vita vya Russia na Ukraine katika usalama wa chakula na vilevile kuitwa umoja kati ya watu wa imani tofauti.

TRT Afrika