Mkuu wa Polisi nchini Kenya Japhet Koome amejiuzulu nafasi yake ya Inspekta Jenerali Polisi.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Kenya, imesema kuwa Rais William Ruto amekubali kujiuzulu kwa Koome.
Nafasi ya Inspekta Jenerali Polisi hivi sasa inakaimiwa na Douglas Kanja ambae alikuwa naibu wake.
Wakati huo huo, Rais Ruto ameteua manaibu wawili watakaokaimu nafasi ya naibu inspekta jenerali, ambao ni Eliud Lang’at na James Kamau.
Rais pia amefanya mabadiliko katika uongozi wa magereza kwa kumfuta kazi John Wariouba ambae Ikulu inasema amechukua likizo ya lazima kabla ya muda wake kuisha.
Kutokana na taarifa hiyo, Mkuu mpya wa Magereza nchini Kenya hivi sasa ni Patrick Mwiti Arandu.
Hatua hii, inakuja, siku moja tu baada ya Rais Ruto kutengua baraza la mawaziri nchini humo.
Mabadiliko hayo, ni sehemu ya ahadi aliyoitoa rais Ruto kwa wananchi baada ya kupata shinikizo la kutakiwa kufanya mabadiliko serikalini, ikiwemo yeye mwenyewe kutakiwa kujiuzulu.