Rais wa Kenya, William Ruto, alifika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta kwa gari ndogo la umeme, tofauti na msafara wa kawaida wa serikali wenye magari yanayotumia mafuta ya petroli. Anahudhuria Mkutano wa mabadiliko ya Tabia Nchi.
Rais wa Kenya, William Ruto, alizindua kikao cha mawaziri siku ya Jumatatu huku zaidi ya viongozi wa nchi kadhaa wakianza kuwasili, wakiwa na nia ya kuwa na sauti kubwa zaidi kimataifa na kupata ufadhili na msaada.
"Huu si mkutano wa kawaida. Hatujakuja hapa tu kujadili Afrika au mabadiliko ya hali ya hewa kwa njia ya kawaida, ambayo mara nyingi inaonyesha tofauti zetu - kaskazini dhidi ya kusini, nchi zilizoendelea dhidi ya zinazoendelea, wanaochafua mazingira dhidi ya waathirika," Ruto alisema.
Wasemaji wa kwanza walikuwa vijana, ambao walidai sauti kubwa zaidi katika mchakato huo.
Fursa
"Kwa muda mrefu tumetazama hili kama tatizo. Kuna fursa kubwa pia," Ruto alisema kuhusu mgogoro wa hali ya hewa.
"Tunapaswa kuona katika ukuaji wa kijani siyo tu suala la dharura la hali ya hewa, bali pia chemchemi ya fursa za kiuchumi zenye thamani ya mabilioni ya dola ambazo Afrika na Dunia zimejiandaa kuzitumia," aliongeza.
Uzalishaji mkubwa wa gesi chafu unazalishwa na uchumi wa nchi zilizoendelea, lakini nchi zinazoendelea ikiwemo Afrika zinakumbwa zaidi na athari zake. Lakini Ruto alisema mkutano huo haukuhusu kusajili malalamiko bali kuchunguza fursa.
"Tuna uwezo mkubwa wa nishati mbadala, na rasilimali asilia za kuimarisha matumizi yetu wenyewe, na kuchangia kwa maana kubwa katika kupunguza kaboni katika uchumi wa dunia," kiongozi wa Kenya ambaye hivi karibuni alikosolewa kwa kufuta marufuku ya ukataji miti nchini mwake alisema.
Fedha na Uzalishaji
"Huu ni wakati wetu," Mithika Mwenda kutoka Muungano wa Haki ya Hali ya Hewa ya Afrika alisema kwa kusisitiza kwamba mwenendo wa kila mwaka wa msaada wa hali ya hewa kwa bara hilo ni asilimia kumi au chini ya kile kinachohitajika na ni "sehemu ndogo" ya bajeti ya kampuni zinazochafua mazingira.
"Tunahitaji kuona mara moja utoaji wa dola bilioni 100 zilizoahidiwa (na nchi tajiri kwa nchi zinazoendelea kila mwaka kwa ufadhili wa hali ya hewa)," alisema Simon Stiell, Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa.
Zaidi ya dola bilioni 83 za ufadhili wa hali ya hewa zilitolewa kwa nchi masikini zaidi mwaka 2020, ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na mwaka uliopita lakini bado ni kidogo ikilinganishwa na lengo lililowekwa mwaka 2009, taarifa ya shirika la habari la AFP inasema.
Madhara
"Tuna rasilimali nyingi za nishati safi na mbadala, na ni muhimu kwamba tuitumie kwa ajili ya ustawi wetu wa badae. Lakini ili kuzitumia, Afrika inahitaji ufadhili kutoka kwa nchi zilizoendelea ambazo zimejipatia utajiri kutokana na mateso yetu," Mohamed Adow kutoka Power Shift Africa alisema kabla ya mkutano huo.
Washiriki kutoka nje ya Afrika ni pamoja na mjumbe wa hali ya hewa wa serikali ya Marekani, John Kerry, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye amesema atajadili masuala ya fedha kama moja ya "dhuluma inayowaka ya mgogoro wa hali ya hewa."
Kenya inapata asilimia 93 ya nishati yake kutoka vyanzo vya nishati mbadala na imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ya kutumia mara moja, lakini inakabiliwa na changamoto nyingine za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Changamoto nyingine kwa bara la Afrika ni kuwa na uwezo wa kutabiri na kufuatilia hali ya hewa ili kuzuia vifo na uharibifu wa mabilioni ya dola ambao, kama mabadiliko ya hali ya hewa yenyewe, una athari kubwa zaidi ya bara hilo. "Kunapotokea mwisho wa ulimwengu, itatokea kwa sisi sote," Ruto alionya.