Kizza Besigye wa Uganda alikamatwa nchini Kenya mnamo Novemba 16, 2024. / Picha: Reuters

Mke wa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amesema hatarajii kupata kesi ya haki baada ya kuzuiliwa katika nchi jirani ya Kenya, kurudishwa nyumbani na kutuhumiwa kumiliki silaha na makosa mengine katika mahakama ya kijeshi.

Winnie Byanyima alisema wiki iliyopita mumewe alikamatwa alipokuwa akijiandaa kuhudhuria uzinduzi wa kitabu jijini Nairobi mnamo Novemba 16 - katika kile ambacho shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International na afisa mkuu katika wizara ya mambo ya nje ya Kenya wameeleza kuwa ni utekaji nyara.

Msemaji wa serikali ya Uganda, Chris Bar yomunsi, alisema wiki iliyopita nchi yake haifanyi utekaji nyara, na kwamba ukamataji nje ya nchi ulifanyika kwa ushirikiano na nchi mwenyeji, lakini hakuzungumzia kisa hicho maalum.

"Katika mahakama ya kijeshi, hatutarajii kupata haki," Winnie Byanyima aliambia Reuters katika mahojiano mjini Kampala siku ya Jumamosi.

'Imani na mahakama'

"Tunaweza tu kusubiri wafike katika mahakama ya kiraia," aliongeza Byanyima, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNAIDS.

Byanyima alisema mashtaka hayo yamechochewa kisiasa na kumtaka Rais Yoweri Museveni "kusimama na kutafakari, kwa sababu suluhisho hili la kuharamisha na kuondoa upinzani kwa njia ya uhalifu ni kosa."

Msemaji wa jeshi la Uganda Felix Kulayigye alipuuzilia mbali kauli yake, akisema mahakama itafuata sheria.

"Tuna imani na mahakama," alisema. "Mahakama inazingatia sheria na kanuni za nchi. Imetolewa katika mfumo wetu wa mahakama kama nchi na inatoa haki kwa ufanisi na uadilifu."

Washirika wa zamani

Besigye wakati mmoja alikuwa mshirika na daktari wa kibinafsi wa Museveni wakati kiongozi huyo mzee alikuwa msituni akipigana na serikali ya wakati huo katika miaka ya 1980.

Wanaume hao wawili walitofautiana na Besigye aliendelea na changamoto na kushindwa na Museveni katika chaguzi nne za urais, kila mara akikataa matokeo kama ya udanganyifu.

Upinzani na wanaharakati wa haki za Uganda kwa muda mrefu wamekuwa wakiishutumu serikali ya Museveni kwa kutumia mahakama ya kijeshi kuwaadhibu wapinzani wa kisiasa, madai ambayo serikali inakanusha.

Byanyima alisema alimtembelea mume wake gerezani na alimweleza kuwa alisikia watu waliomchukua wakizungumza lugha ya Kiganda, na kumfanya ajitambue kuwa ni Waganda.

TRT Afrika