Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Hivi karibuni, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) ilitangaza kuwa inashindwa kusikiliza kesi zake kutokana na ukosefu wa fedha.
"Kutokana na michango duni kutoka kwa nchi wanachama, Mahakama ilishindwa kuendesha shughuli zake za mwezi Mei 2024 na mwezi Juni," ilisomeka sehemu ya taarifa ya Mahakama hiyo inayoketi jijini Arusha nchini Tanzania.
Kulingana na EACJ, changamoto hiyo ya kifedha inatatiza shughuli za utoaji haki ambayo ni moja ya majukumu ya mahakama hiyo.
Siku chache baadaye, kukaibuka taarifa za Bunge la Afrika Mashariki (EALA) nalo kulazimika kusogeza mbele baadhi ya shughuli zake kwa sababu kama hizo.
Wakati Bunge hilo likijiandaa kujadili bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Juni 23, 2024, ni dhahiri kuwa ufinyu wa bajeti umetatiza baadhi ya shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria.
"Kumekuwa na mabadiliko kwenye baadhi ya shughuli za kamati, marekebisho ya baadhi ya shughuli za kamati, lakini hatujaahirisha kabisa japo ni kweli tunakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na baadhi ya nchi washirika kuchelewa kutuma fedha," Nicodemus Ajak Bior, afisa habari mwandamizi anaiambia TRT Afrika.
Muenendo usioridhisha wa nchi wananchama kuwasilisha michango yao kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa sasa.
Baadhi ya wabunge wa EALA, wanaharakati na watu kutoka kada mbalimbali wametaka nchi zinazishindwa kutimiza sharti hilo la kisheria, kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo.
Kila nchi mwanachama ilipaswa kuwa imechangia dola milioni 7.35 kwa mwaka huu wa fedha, hata hivyo, kulingana na mchanganuo wa michango hiyo.
Hata hivyo, hadi kufikia Juni 6, 2024, Burundi ilikuwa inadaiwa dola milioni 11.2 huku DRC ikiwa bado haijachangia chochote.
Nchi hiyo inayosifika kwa utajiri wa maliasili, hasa ya madini inadaiwa dola milioni 14.7 kama mchango wake kwa jumuiya hiyo.
Katika ya nchi nane za EAC, ni Kenya pekee iliyofanikiwa kumaliza michango yake kwa asilimia 100, ikiwa inadaiwa shilingi 20 tu hadi sasa.
Tanzania inafuata kwa karibu ikiwa imelipa dola milioni 7,229,430, ambayo ni sawa na asilimia 98 ya deni zima la dola milioni 7.35.
Rwanda, ambayo inasifika kuwa na uchumi mzuri, inadaiwa dola 920,869, ikiwa imeshalipa dola milioni 6,431,255.
Nchi ya Uganda bado ina deni la dola milioni 7,151,921 baada ya kuwa imechangia dola 200,203 wakati Sudan Kusini ina deni la dola milioni 6,093,993.
Kwa ujumla, deni zima la nchi wanachama wa Jumuiya hiyo hadi kufikia Juni 6, ni dola milioni 35.7.