Ripoti ya polisi ilisema kuwa dawa hizo zililengwa kusambazwa katika miji ya Mombasa na Nairobi./ Picha : Ofisi ya mwendesha mashtaka

Mahakama nchini Kenya imemtolea kifungo cha miaka 45 jela, raia wa Tanzania aliyekutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine.

Maimuna Jumanne Amir alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi mnamo Machi 2021, akiwa na zaidi ya kilo 5 za heroine yenye thamani ya Ksh.16,167,000. ($100.72).

''Hakimu Mfawidhi Martin Rabera alimkuta Maimuna Jumanne Amir na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya gramu 5,389 za heroine zilizofichwa kwenye begi nyeusi ya kusafiria,'' ilisema sehemu ya taarifa ya ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hukumu ya mtuhumiwa huyo iligawanywa kwa makosa mawili, moja ikiwa kusafirisha dawa za kulevya na ya pili kupatikana amebeba dawa za kulevya.

Sheria kali ya kudhibiti dawa za kulevya

Maimuna alikamatwa mwaka 2021 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi, Mombasa, ambapo anaaminiwa alianzia safari yake nchini Afrika Kusini, akapitia Addis Ababa na kutua mjini Mombasa.

Dawa hizo zailizogawanya katika mifuko kadhaa nyeusi za plastiki na kisha kumiminiwa juu bizari nyembamba na pilipili kufunika harufu yake, zilifichwa katika kitambara cha ndani cha sanduku lake.

Ripoti ya polisi ilisema kuwa dawa hizo zililengwa kusambazwa katika miji ya Mombasa na Nairobi.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mombasa Martin Rabera, katika uamuzi wake, alimhukumu kifungo cha miaka 35 jela kwa ulanguzi wa dawa za kulevya, na miaka 10 ya ziada kwa kupatikana na dawa za kulevya.

Kifungo cha miaka kumi (Cha kukutwa na dawa za kulevya) hata hivyo kinatozwa faini mbadala ya Ksh.48 milioni.

“Mshtakiwa alitozwa faini ya Ksh.48,501,000 (mara tatu ya thamani ya dawa alizokuwa nazo), akikosa kulipa faini hiyo, atatumikia kifungo cha miaka 10 jela kwa kosa la kubeba dawa za kulevya, kinyume na Kifungu cha 4(a) cha Madawa ya Kulevya, Sheria ya udhibiti wa dawa za kulevya Na. 4 ya 1994," ilisema ofisi ya Mkurugenzi w aMashtaka- ODPP.

Janga la Kitaifa

Maimuna anaaminiwa kufanya kosa hilo pamoja na washukiwa wengine ambao hawakuwa mahakamani.

Wakati akitoa hukumu hiyo, Hakimu Rabera alisema kuwa ofisi ya mwendesha mashtaka iliweza kubainisha kesi hiyo mbele ya mahakama, bila shaka yoyote kwa kuwaleta mashahidi 16.

Utumiaji wa dawa za kulevya katika pwani ya Kenya, umelaumiwa kwa kudorora kwa utenda kazi wa vijana wanaoangukia 'uteja' hali ya kuwa tegemezi kamili kwa dawa hizo.

Uteja umesababisha umaskini mkubwa katik aeneo hilo.

Wakati huo huo, uuzaji wa dawa hizo umesababisha kuibuka kwa makundi ya matendo ya kihalifu ikiwemo 'Mafia' na majambazi.

Kenya ilifanyia mabadiliko sheria yake ya udhibiti wa dawa za kulevya mnamo Machi 2022, ambapo imeweka hukumu kali zaidi kwa watuhumiwa ikiwemo faini ya hadi milioni mia moja na vifungo vya maisha kwa baadhi ya mashtaka.

TRT Afrika