Rais William Ruto amemteua Naibu Rais mpya baada ya Rigathi Gachagua kuondolewa na Bunge la Seneti.
"Rais William Ruto amependekeza na kulipeleka bungeni jina la Profesa Kithure Kindiki kama Naibu Rais," taarifa ya Ikulu ya Kenya imesema.
"Iwapo itaidhinishwa, Waziri wa Mambo ya Ndani atamrithi Rigathi Gachagua ambaye alitimuliwa na Seneti siku ya Alhamisi," imeongeza kusema taarifa hiyo.
Kithure Kindiki ni nani?
Kindiki ni mwanasiasa wa Kenya na wakili maarufu ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa.
Alizaliwa Julai 16, 1972 huko Tharaka, kaunti ya Tharaka Nithi.
Alisoma Shule ya Lenana, kabla ya kwenda Tharaka Boys High. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 52 alihitimu Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Moi mwaka wa 1998.
Aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini ambako alipata Shahada ya Uzamili mwaka 2000.
Miaka miwili baadaye, wakili huyo anayefahamika kwa ufasaha wake alifuzu shahada ya uzamivu katika Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini.
Kithure aliwahi kuwa mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Moi kati ya 1999 hadi 2003 na baadaye akawa mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi kati ya 2004 na 2005.
Amehudumu kama wakili mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kama wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya tangu 2001.
Kindiki alijiunga rasmi na ulingo wa kisiasa mwaka wa 2013 alipochaguliwa kuwa seneta wa kwanza wa Tharaka Nithi.
Alihudumu kama Kiongozi wa Wengi katika Seneti katika muhula wake wa kwanza, kati ya 2013 - 2017. Mnamo 2017, alichaguliwa tena na wenyeji wa kaunti ya Tharaka Nithi na kuhudumu kama Naibu Spika wa Bunge kutoka 2017 hadi 2020 kabla ya kuondolewa katika nafasi ya chama cha Jubilee.
Katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022, Kindiki alikuwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Ruto lakini bahati haikuwa yake.
Rigathi Gachagua akiendelea kupata nafuu kutokana na maumivu makali ya kifua yaliyomzuia kufika Bunge la Seneti kujitetea, zamu ya kindiki hatimae imewadia.
Bunge la Taifa linajadili hoja hiyo
"Spika, umewasilisha ujumbe kutoka kwa Rais Ruto kuhusu uteuzi wa Kithure Kindilki kujaza nafasi ya ofisi ya Naibu Rais. Tafadhali toa muongozo ili uteuzi ufanyike leo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Rais leo," Jane Wangechi Kagiri Mbunge wa Laikipia Kaunti amesema bungeni.
"Ukimtazama aliyeteuliwa (Kindiki), tulimkagua sio zaidi ya miezi 2 iliyopita, na hiyo inamaanisha sio zaidi ya miezi 6. Kwa nini tusitumie mwendo sawa na tuliyotumia hivi majuzi? Tunaweka tu hoja na swali na tunamaliza kumpitisha leo," David Kipalgat Mbunge wa Baringo amesema.
Maoni ya wananchi
Kuteuliwa kwa Kithure Kindiki kumezua hisia tofauti nchini
" Tunamuomba Rais Ruto asimtumie Kithure Kindiki vibaya kwa sababu Kindiki ni mpole sana," mkazi wa kaunti ya Nakuru amesema.
Naye Emmanuel Asinza kutoka Nairobi ameiambia TRT Afrika:
"Mimi sijafurahia vile wamemuondoa Gachagua, hata akiwa hospitalini, wangengoja hata apone kwanza. Kindiki si mtu mbaya lakini wangengoja Gachagua apone."
Cynthia Atieno wa Monbasa ameiambia TRT Afrika anachojali ni maendeleo.
"Wanasiasa wote ni kitu kimoja tu hakuna tofauti. Swali langu ni serikali ambayo tulichagua itaanza kufanya kazi lini kwa sababu wamekuwa katika siasa tu tangu 2022."
Mbunge wa Kajiado Tindi mwale amesema, " Rais Ruto amefanya vyema kumteua Kithure Kindiki kwa sababu atafanya kazi yake vyema na hataangazia mazungumzo ya ukabila."