Kwa sasa Rais Museveni anaongoza katika sheria ambayo haina masharti ya muda wa uongozi , ila ni muhula wa miaka mitano, mitano/ Picha: Reuters 

Kiongozi wa zamani wa Upinzani nchini Uganda, Mathias Mpuuga ameeleza mageuzi matano ya sheria ya uchaguzi anayokusudia kuyawasilisha Bungeni wiki ijayo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026 .

"Moja ya eneo muhimu ni urejeshaji wa mipaka ya muda wa urais. Tumezungumza kuhusu hili kwa njia tofauti. Ni jambo ambalo limetia doa taifa hili. Ukomo wa muda ulikuwa ni kati ya makubaliano ya Katiba ya 1995. Dhamira ilikuwa kuipa nchi nafasi kwa mara ya kwanza kabisa katika historia yetu kubadili uongozi katika uchaguzi huru na wa haki," Mpuuga amesema.

Mwaka wa 2005, Bunge la Uganda lilifanyia marekebisho katiba ili kuondoa ukomo wa mihula ya urais, kuruhusu walio madarakani kugombea tena kwa muda usiojulikana.

Mnamo 2017, wabunge walipiga kura kwa wingi kufuta kifungu cha ukomo wa umri wa urais kinachohitaji kuwa wagombea urais wawe na umri wa chini ya miaka 75. Hii ilimruhusu Rais Yoweri Museveni, kuendelea kugombea urais.

Pia amepedendekeza marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ya Rais ili kuruhusu wapiga kura kwenda mahakama za rufaa wasiporidhika ili kupunguza hamu ya Serikali ya kuwaweka wagombea urais kizuizini.

Kiongozi wa zamani wa Upinzani, Mathias Mpuuga anataka sheria za uchaguzi zibadilishwe / Picha Parliament Watch

Dkt. Kizza Besigye alimpinga rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 na hatimae kukamatwa. Hayo pia yalimtokea Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine aliyegombea kiti cha urais 2021.

Hata hivyo, amependekeza kuwa walalamishi watahitajika kuweka dhamana mahakamani, ili kuhakikisha kuwa baadhi ya walalamishi hawapotezi muda wa mahakama.

Mpuuga pia anataka mabadiliko yafanywe kupunguza ukubwa wa bunge, kuruhusu wafungwa na raia walioko Diaspora kupiga kura.

TRT Afrika