Mbunge wa Uganda Dkt. Ayume Charles amebaini kuwa wagonjwa 100 nchini Uganda wanaofaa kupandikizwa figo wamekwama kufuatia Serikali kushindwa kuunda Baraza la Upandikizaji Viungo.
Mbunge huyo alimuomba Waziri Mkuu wa nchi Robinah Nabbanja kuelezea kwa nini serikali haijaunda Baraza la Upandikizaji Viungo, lenye jukumu la kusimamia shughuli zote za upandikizaji wa viungo nchini.
“Kwa sasa kuna mrundikano wa wagonjwa zaidi ya 100 wanaohitaji huduma ya kupandikizwa figo. Kikwazo pekee ni uteuzi na uendeshaji wa Baraza la Kupandikiza viungo. Je, ni lini serikali itaunda na kulifanyia kazi Baraza hilo ili kuokoa maisha na kupunguza utalii wa kimatibabu hasa kwa wale ambao hawawezi kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya huduma za upandikizaji?” aliuliza Dkt. Ayume.
Waziri Mkuu alikiri wasiwasi wa Dkt. Ayume.
"Mahitaji ya bajeti ya kuanzishwa kwa Baraza hili ni zaidi ya dola milioni 1.9 (UGX7.2Bn). Kati ya fedha hizo, zaidi ya dola milioni 1.3 (Shs5Bn) ziliombwa mwaka huu wa fedha na Wizara ya Afya," Waziri Mkuu Robinah Nabbanja alielezea.
"Fedha hizi zitakapotolewa na Wizara ya Fedha, Baraza la Uchangiaji na Upandikizaji wa Uganda litaundwa. Wajumbe saba wametambuliwa kwa ajili ya kuteuliwa,” Nabbanja alielezea.
Wasiwasi wa matibabu ya figo umekuja baada ya Waziri wa Afya, Dkt. Ruth Aceng mnamo Aprili 2024, kutangaza kusitisha shughuli zote za upandikizaji wa viungo vya Binadamu kutokana na kushindwa kwa Serikali kutoa zaidi ya dola milioni 1.3 (Shs5Bn) kwa ajili ya Baraza la Upandikizaji viungo.
Wakati huo, Wizara ya Afya ilibainisha kuwa kati ya fedha zinazohitajika zaidi ya dola 978,204 ( Sh3.6Bn) zinahitajika kwa ajili ya mafunzo kutoka mataifa mengine, ambapo zaidi ya dola 380,413 ( Sh1.4Bn) ni kwa ajili ya uendeshaji wa Baraza la Kupandikiza viungo.