Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa alitoa wito kwa wanachama wa harakati ya nchi zisizofungamana na siasa za upande wowote mjini Kampala, Uganda, kuweka shinikizo kwa Israel kutekeleza usitishaji vita huko Gaza baada ya siku 100 za vita dhidi ya kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas.
Rayid Mansour alihutubia katika hotuba yake ya ufunguzi wanachama 120, waliokutana wiki nzima hii, kwamba licha ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na maazimio ya Baraza la Usalama, usitishaji wa mapigano ulisalia kuwa ngumu.
"Bado tuko chini ya uvamizi huu wa kikoloni na Israel na tunaona mauaji ya kimbari yakifanywa kwa watu wetu, hasa katika Ukanda wa Gaza," alisema balozi Mansour.
Alisema Wapalestina wanaishukuru Afrika Kusini kwa kuanzisha kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki. "Sisi ndio wa mwisho wa kupigania uhuru wetu. Ninyi nyote mlitimiza uhuru wenu wa kitaifa na kukomesha ukoloni.” aliongeza Mansour.
Kwa upande wake mataifa ya kiarabu yameahidi kusukuma ajenda ya Palestine hadi amani irejee Gaza inayozingirwa.
Somalia nayo imesisitiza kuwa inataka utambulisho wa mipaka yake na heshima kwa uhuru wake kwa wanachama wote.
Somalia imejikuta ikitafuta kuungwa mkono katika kuikashifu Ethiopia kwa kusaini makubaliano na eneo linalojitangazia kujitenga la Somaliland, huku Somalia ikisema huo ni ukiukaji wa uatawala wake huru.
Vuguvugu la NAM lililoundwa wakati wa kuporomoka kwa mifumo ya kikoloni na katika kilele cha Vita Baridi, limekuwa na sehemu muhimu katika michakato ya kuondoa ukoloni, kulingana na tovuti yake.
Takriban marais 30 wanachama wa vuguvugu hilo wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi mwishoni mwa mijadala ya wiki nzima. Rais wa Uganda Yoweri Museveni atapokea uenyekiti wa vuguvugu hilo kwa muda w amiaka mitatu kutoka kwa rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev.