Maria Sarungi-Tsehai anafanya kampeni za mabadiliko ya kisiasa, uhuru wa kujieleza na haki za wanawake nchini Tanzania. / Picha: Maria Sarungi-Tsehai

Mwanaharakati mashuhuri wa haki wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai ameripotiwa kuachiliwa baada y akutekwa nyara kwa saa kadhaa akiwa nchini Kenya.

Katika video iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa X, Tsehai amethibitisha kuwa alitekwa lakini akaahidi kutoa maelezo zaidi baadaye.

''Asanteni sana, niko salama, Mungu ni mwema na kesho nitachukua muda niwashukuru vizuri, Nawashukuru watu wa Kenya, watu wa Tanzania na Kimataifa,'' alisema Sarungi.

katika video hiyo, Sarungi aliyeonekana ameambatana na watu wengine wanne, aliangua kilio akisema sasa yuko salama.

''Natoa shukrani zaidi kwa walionipigania, kwasababu leo nimeweza kuokolewa salama....'' aliendelea kusema.

Tsehai anadaiwa kutekwa nyara katika mitaa ya mji mkuu wa Kenya Nairobi siku ya Jumapili, shirika la Amnesty International na shirika lake lilisema.

Tsehai anafanya kampeni za mabadiliko ya kisiasa, uhuru wa kujieleza na haki za wanawake nchini Tanzania na ana wafuasi milioni 1.3 kwenye X.

Shirika la Amnesty tawi la Kenya lilisema "alitekwa nyara na watu watatu waliokuwa na silaha kwenye gari nyeusi (Toyota) Noah" mwendo wa saa tisa mchana katika eneo la Kilimani katikati mwa Nairobi.

Shrika lake Tsehai, Change Tanzania, liliandika kwenye X: "Tunaamini waliomteka nyara ni sehemu ya mawakala wa usalama wa Tanzania wanaofanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania kunyamazisha... ukosoaji halali."

'Ujasiri katika kutetea haki'

"Ujasiri wake wa kutetea haki umemfanya kuwa shabaha, lakini hatutaruhusu wakati huu kunyamazisha sauti yake," liliongeza shirika lake.

Tanzania imeshudia mvutano kati ya upinzani na vyombo vya usalama katika miezi ya hivi karibuni, huku viongozi wa upinzani walioandaa maandamano wakikamatwa kwa kile serikali inadai ni kutofuata taratibu na kukaidi agizo la polisi.

Rais Samia Suluhu Hassan alitunukiwa awali kwa kuboresha haki za kidemokrasia baada ya kuchukua nafasi ya mtangulizi wake John Magufuli mwaka 2021.

Lakini Kumekuwa na malalamiko kadhaa kutoka upinzani na mashirika ya haki pamoja na serikali za Magharibi kukosoa kile wanachokiona kama ukandamizaji mpya, ikiwa ni pamoja na kukamatwa, utekaji nyara na hata mauaji ya viongozi wa upinzani.

Serikali imekanusha kwa kauli kali kuhusika na matendo hayo ya ukandamizaji na kudai kuwa inafanya kila juhudi kuwakamata wahusika.

TRT Afrika