Spika wa Bunge la Uganda Anita Among amewekewa vikwazo na Marekani na Uingereza/ Picha: Anita Among

Marekani imewawekea vikwazo maafisa wa serikali ya Uganda watano wa sasa na wa zamani kwa madai kuwa wamehusika katika ufisadi mkubwa au ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

"Spika wa Bunge Anita Among amewekewa vikwazo kutokana na kuhusika katika ufisadi mkubwa unaohusishwa na uongozi wake wa Bunge la Uganda," taarifa kutoka serikali ya Marekani imesema.

"Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Karamoja, Mary Goretti Kitutu, Waziri wa zamani wa Mambo ya Karamoja Agnes Nandutu, na Waziri wa Fedha, Amos Lugolobi wanateuliwa kuwekewa vikwazo kutokana na kuhusika katika ufisadi mkubwa unaohusiana na matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kutorosha vifaa kutoka kwa wahitaji wa Uganda," taarifa hiyo imesema.

Maafisa wote wanne wanadaiwa kutumia vibaya nyadhifa zao za umma kwa manufaa yao binafsi kwa gharama ya wananchi,

Peter Elwelu, Naibu Mkuu wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), amewekewa vikwazo kwa madai ya  kuhusika kwake katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu/ Picha:UPDF

Vikwazo hivyo pia vimelenga afisa wa jeshi.

"Zaidi ya hayo, Peter Elwelu, aliyekuwa naibu mkuu wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), ameteuliwa kutokana na kuhusika kwake katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Hasa, Peter Elwelu alihusika, wakati akiongoza vikosi vya UPDF, katika mauaji ya kiholela ambayo yalifanywa na wanachama wa UPDF," taarifa imeongeza kusema.

Kutokana na hatua hizi, maafisa waliowekewa vikwazo hawataruhusiwa kuingia Marekani.

Idara hiyo pia imesema itachukua hatua za kuweka vikwazo vya viza kwa maafisa wengine wa Uganda kwa kudhoofisha mchakato wa kidemokrasia na kukandamiza watu waliotengwa au walio hatarini nchini Uganda.

Inadai kuwa watu hawa wanawajibika, au wanashiriki katika, ukandamizaji wa wanachama wa Uganda wa makundi ya upinzani ya kisiasa, waandaaji wa mashirika ya kiraia, na jumuiya zilizo hatarini nchini Uganda.

Vikwazo kutoka Uingereza

Spika wa Bunge Anita Among mwanachama mkuu wa chama tawala cha Uganda, NRM na mshirika wa Rais Yoweri Museveni.

Amekuwa chini ya uangalizi hivi karibuni kuhusu chanzo cha utajiri wake pamoja na madai yanayohusiana na matumizi mabaya ya rasilimali za bunge. Uingereza ilitangaza vikwazo dhidi yake Aprili 2024, ikidai fedha alizipata kwa njia ya rushwa.

Lakini Among amepinga madai hayo baada ya Rais Museveni kumtaka aweke wazi ni mali gani anamiliki Uingereza.

"Nyumba inayosemekana ni yangu huko Uingereza yenye anwani ya Kiwanja Flat 4, Silk House, 7 Barabara ya Waterden, London, E20 3AL, Uingereza, ambayo walimjulisha Rais kuwa inamilikiwa na mimi mwenyewe, hakika ina mmiliki ambaye amesajiliwa katika mfumo wao (Serikali ya Uingereza), na mmiliki huyu, kulingana na rekodi zao, sio Anita Among," Spika wa Bunge alisema katika taarifa.

"Kiini cha kweli cha suala hili ni kumlenga Anita Among kwa kuwa na sauti dhidi ya ushoga. Mengine ni vizingizio," amesema.

Mbali na spika wa Bunge, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Karamoja, Mary Goretti Kitutu, Waziri wa zamani wa Mambo ya Karamoja Agnes Nandutu pia waliwekewa vikwazo.

TRT Afrika