#HTD38 : Rais Ali Bongo akiongea na Bunge / Photo: AFP

Uhuru wa nchi

Gabon ni nchi inayopatikana katika eneo la Afrika ya Kati na ina mipaka na Kongo Brazzaville, Equatorial Guinea na Cameroon.

Gabon ilipata uhuru wake mnamo Agosti 17, 1960. Ilitawaliwa na Ufaransa na kuingizwa katika koloni la Kongo ya Ufaransa mnamo 1882 na kisha kuwa koloni tofauti mnamo 1906.

Ukubwa wa Gabon

Ardhi ya nchi ina jumla ya eneo la 267,670 km² (103,348 mi²) na ufuo wa jumla wa kilomita 885 (549.9 mi).

Kwa hiyo Gabon ni nchi ya 30 ndogo zaidi barani Afrika na mojawapo ya nchi zilizo na watu wachache zaidi duniani. Idadi kubwa ya watu wanaishi katika maeneo ya mijini haswa mji mkuu Libreville.

Uongozi

Taifa hilo dogo la Afrika ya kati limetawaliwa na familia moja kwa zaidi ya miaka 55 kati ya miaka 63 tangu lipate uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960. Rais wa kwanza wa nchi hiyo alikuwa Leon Mba aliyefariki mwaka 1967.

Ali Bongo, 64, ambaye alikuwa anawania muhula wa tatu katika uchaguzi wa Jumamosi, alichukua hatamu wakati babake Omar alipofariki mwaka 2009 baada ya takriban miaka 42 madarakani.

Bongo, ambaye alichukua wadhifa huo mwaka wa 1967, alikuwa na sifa ya kleptocrat - mmoja wa watu tajiri zaidi duniani, akiwa na utajiri unaotokana na utajiri wa mafuta wa Gabon.

Mwanae alikua anachukuliwa kama msaidizi wa familia hiyo tajiri inayotawala na wakati mmoja alijulikana na kwa kifupi kama ABO, Ali B -- au, "Monsieur Fils" (Bwana Mwana).

Mnamo Oktoba 2018, Bongo alipata kiharusi ambacho kilimuathiri kwa miezi 10. Kipindi hicho kilichochea madai kuwa hafai kutawala na kuchochea jaribio dogo la mapinduzi.

Gabon ina mfumo wa rais wa serikali. Mabadiliko ya katiba ya hivi majuzi kufuatia kura ya maoni yalimruhusu Rais Ali Bongo kuwania muhula wa tatu madarakani.

Nchi tajiri

Gabon ni mojawapo ya nchi tajiri zaidi barani Afrika katika suala la Pato la Taifa kwa kila mtu, kutokana na mapato ya mafuta na idadi ndogo ya watu milioni 2.3, shirika la habari la AFP linaripoti.

Katika miaka ya 1970, nchi iligundua akiba nyingi za mafuta katika fuo za bahari yake , na kuiruhusu kujenga tabaka la kati lenye nguvu na kupata jina la "emirate ndogo ya Afrika ya kati". Mafuta yanachangia asilimia 60 ya mapato ya nchi.

Lakini theluthi moja ya watu bado wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa dola 5.50 kwa siku, kulingana na Benki ya Dunia.

Juhudi za uhifadhi

Misitu inafunika asilimia 88 ya ardhi ya Gabon, ikitoa mazingira nzuri kwa sokwe, nyati, chui weusi, tembo, sokwe na spishi zingine.

Nchi, ambayo inajitangaza kama "bustani la Edeni la mwisho", imekuwa mtetezi mkuu wa uhifadhi katika eneo ambalo wanyamapori wanakumbwa na vita, uharibifu wa makazi na biashara ya wanyama porini.

Mnamo 2002, ilianzisha mtandao wa mbuga 13 za kitaifa zinazochukua asilimia 11 ya eneo lake.

Moja ya mafanikio yake makubwa ni uhifadhi wa tembo wa misitu wa Kiafrika walio katika hatari ya kutoweka. Idadi yao ya kimataifa imepungua kwa asilimia 86 katika miaka 30 lakini nchini Gabon wameongezeka mara mbili katika muongo mmoja.

Gabon ni nchi yenye misitu na wanyama na mimea iliyohifadhiwa na kulindwa katika mbuga kumi na tatu zikiwemo mbuga za kitaifa za Lope na Ivindo ambazo zimeorodheshwa kama Maeneo ya Urithi wa Dunia wa UNESCO.

TRT Afrika