Mke wa rais wa Gabon aliyeondolewa madarakani na majeshi Ali Bongo Ondimba, amefungwa jela, wakili wake alisema Alhamisi.
Sylvia Bongo Ondimba Valentin, anayedaiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma, alifungwa jela siku ya Jumatano. Wakili wake Francois Zimeray alilaani "utaratibu huo wa kiholela...haramu".
Mumewe Ali Bongo, aliyekuwa rais wa Gabon yupo chini ya kifungo cha nyumbani tangu mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika ya kati mwishoni mwa Agosti.
Sylvia Bongo Ondimba Valentin, mke wa Bongo alishtakiwa Septemba 28 kwa utakatishaji fedha, kughushi nyaraka na kughushi rekodi.
Sylvia Bongo amekuwa katika kizuizi cha nyumbani katika mji mkuu, Libreville, tangu mapinduzi ya Agosti 30 yalipoondoa uongozi wa miaka 55 ya utawala wa Bongo.
Matokeo ya kura zilizoghushiwa
Wapinzani hao wanadai kiongozi huyo wa zamani wa nchi na waliomuunga mkono walighushi matokeo ya uchaguzi.
Wanamshutumu Sylvia Bongo na mwanawe, Nourredin Bongo Valentin, kwa kumdanganya rais huyo wa zamani, ambaye hajapona kabisa kutokana na kiharusi kikubwa mwaka wa 2018.
Wanasema kuwa wawili hao wameendesha nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kwa muda wa miaka mitano iliyopita na wametumia vibaya pesa za umma.
Nourredin Bongo Valentin amewekwa kizuizini tangu mapinduzi hayo, akishtakiwa kwa rushwa. "Tulilaani utaratibu huu haramu," wakili Zimeray alisema.
Mapinduzi ya Ali Bongo
Bongo, 64, ambaye alitawala nchi hiyo ya Afrika ya kati tangu 2009, alipinduliwa na viongozi wa kijeshi muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais.
Wengi waliona ni kitendo cha ukombozi badala ya mapinduzi ya kijeshi.
Ali Bongo alichaguliwa baada ya babake Omar Bongo kufariki mwaka 2009 baada ya kuongoza takriban miaka 42 madarakani.
Gabon ni taifa la tatu kwa utajiri barani Afrika katika suala la pato la taifa kwa kila mtu lakini mtu mmoja kati ya watatu anaishi chini ya mstari wa umaskini, kulingana na Benki ya Dunia.