Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kimetangaza kitaanza kutoa mafunzo ya uzamivu mwaka 2025 kwa somo la Kiswahili / Picha: AFP

Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kitaanza kutoa programu za Uzamivu katika lugha ya Kiswahili, kuanzia mwaka wa masomo wa 2025.

Hatua hii inafuatia maamuzi ya Bunge la nchi hiyo kupitisha Muswada wa Baraza la Kiswahili la Kitaifa la Uganda 2023.

Boaz Mutungi, Mhadhiri, Idara ya Lugha za Kiafrika (Kiswahili) katika Chuo Kikuu cha Makerere alisema haya mbele ya Kamati ya Bunge ya Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii wakati akiwasilisha maoni ya idara hiyo kuhusu muswada huo pendekezwa.

Baraza la Kiswahili la Taifa la Uganda linataka kuanzisha chombo kitakachosimamia ukuzaji na udhibiti wa matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Uganda.

Maafisa wa Chuo cha Makerere walikataa pendekezo hilo katika ibara ya 6(1) inayotaka kuweka uanachama wa baraza kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) pekee, wakitaka kuwe na fursa ya kwa vikosi vingine kama vya Polisi kuingia katika Baraza katika kipindi fulani.

Chuo Kikuu cha Makerere pia kilitoa wito wa kujumuishwa kwa viongozi wa kidini katika Baraza la Kiswahili la Taifa la Uganda kikisema kuwa shule nyingi nchini humo zina historia za kidini, ambayo itakuwa na jukumu muhimu katika kupitishwa kwa matumizi ya Kiswahili nchini Uganda.

“Ongeza mwakilishi mmoja kutoka mashirika ya kidini kama kupitia baraza la dini mbalimbali la Uganda. Mashirika yenye misingi ya kiimani ni muhimu katika mifumo yetu ya elimu kwa vile ni vyombo vya msingi vya taasisi nyingi za elimu,” aliongeza Dkt Mutungi.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika