Mahakama ya kesi ndogo ilianzishwa nchini Kenya chini ya Sheria ya Mahakama ya Kesi Ndogo, 2016. Nia yake ilikuwa ni kutatua migogoro yenye thamani ya chini ya KSh1 milioni na kuhakikisha inaweza kutatuliwa kwa haraka kwa kutumia taratibu nyepesi.
"Hadi kufikia wiki iliyopita, ( mwezi Februari) kesi 61,269 zilikuwa zimewasilishwa tangu kuanzishwa kwa Mahakama Ndogo za Madai. Kati ya hizo, mashauri 50,666 yametatuliwa kwa mafanikio makubwa, imaanisha kwamba kwa sasa tuna mashauri 10,603 ambayo yanaendelea katika Mahakama Ndogo za Madai," Jaji Mkuu wa Kenya, Martha Koome amesema katika taarifa.
Huduma hiyo ya mahakama ilianza kutolewa katika kaunti kumi na mbili (12) za Kenya. Ambazo ni Nairobi, Kajiado, Kiambu, Uasin Gishu, Machakos & Makueni, Nyeri, Nakuru, Kakamega, Mombasa, Kisumu na Meru.
Mahakimu wapya waliongezwa kwa ajili ya kutatua kesi chini ya mahakama hiyo.
Koome amesema tangu kuanzishwa, mwaka wa 2021/2022 mahakama za madai madogo kote nchini zimeweza kurudisha takriban KSh9.3 bilioni kwa uchumi wa Kenya na hivyo kuongeza urahisi wa kufanya biashara na kuongeza imani ya wawekezaji.
"Kwa kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa haraka, tunawawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kusuluhisha mizozo yao kwa ujasiri, tukikuza mazingira ambayo biashara inaweza kustawi na uhusiano wa kijamii kuimarishwa," Koome ameongezea.
Inafahamika kuwa kufikia Januari 31, 2024, jumla ya wanawake 7,439, wametumia Mahakama hiyo kufungua kesi. Mahakama hizi zimekuwa muhimu kwa wanawake wa Kenya, ambao wengi wao wanaendesha biashara ndogo na za kati.
Tangu kuanzishwa, Mahakama za Madai Madogo kote nchini zimeweza kutoa takriban KSh9.3 bilioni kwa uchumi wa Kenya na hivyo kuongeza urahisi wa kufanya biashara na kuongeza imani ya wawekezaji.