Mahakama kuu nchini Kenya imetupilia mbali mpango wa Serikali kupeleka baadhi ya askari wake kulinda raia nchini Haiti.
''Ahadi ya Kenya ni kutuma maofisa wapatao 1,000 kusaidia kutoa mafunzo na kusaidia polisi wa Haiti kurejesha hali ya usalama nchini humo ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu ya kimkakati,'' ilisema sehemu ya taarifa kutoka Wizara ya mambo nje ya Kenya, Julai 2023.
Hata hivyo katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ya nchi hiyo imesisitiza kuwa baraza la usalama la kitaifa nchini Kenya halina mamlaka yoyote kisheria kutuma maofisa wa polisi kwenye shughuli zozote za kulinda amani nje ya nchi.
" Uamuzi wa baraza la usalama la kitaifa kupeleka maafisa wa polisi nje ya Kenya na hatua nyingine yoyote inayochukuliwa na chombo chochote cha serikali au ofisa wa serikali ni batili," alisema Jaji Mwita katika maamuzi yake.
Hata hivyo, Serikali ya Kenya imeendelea kuutetea mpango huo na kupinga maamuzi ya Jaji Mwita huku ikisisitiza kuwa nchi hiyo sio mgeni kwenye shughuli za kulinda amani barani Afrika, ikitumia mifano ya harakati zake nchini Sudan Kusini, Namibia, Croatia, Liberia, Sierra Leone na nyinginezo.
Hii inakuja wakati makundi ya kihalifu yanashikilia takribani asilimia 80 ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince huku polisi wa nchi hiyo wakionekana kuzidiwa na vitendo vya utekaji nyara na wizi wa kutumia silaha.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa , Haiti, kupitia Umoja wa Mataifa imekuwa ikiomba msaada wa kimataifa kudhibiti uhalifu nchini humo, bila mafaniko yoyote.
Nchi ya Marekani kwa upande wake, imeunga mkono wazo hilo ikisema iko tayari kuisaidia Kenya katika nia hiyo.
Wakati wa ziara yake nchini Kenya Septemba mwaka jana, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd J. Austin III na mwenzake kutoka Kenya walikubaliana kushirikiana katika masuala ya ulinzi.
Mkataba huo ulisisitiza ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili na Marekani kuisaidia Kenya katika shughuli za kurejesha usalama wa raia katika nchi hiyo kutoka visiwa vya Caribbean.
Hata hivyo, mpango huo haukupokelewa vizuri nchini Kenya huku wengi wakidai kuwa maofisa polisi wa wanajiweka katika hatari.
Mwezi Oktoba mwaka 2023, Mahakama Kuu ya Kenya iliitaka Serikali ya Kenya kusitisha zoezi hilo baada ya chama cha Thirdway Alliance kudai kuwa, uamuzi huo haukuidhinishwa na Bunge la nchi hiyo.
" Amri sasa inatolewa kukataza kupelekwa kwa maafisa wa polisi nchini Haiti au nchi nyingine yoyote ile," Jaji Mwita ameongezea katika uamuzi wake,