Mahakama Kuu nchini Kenya imetoa maagizo ya kusimamisha utekelezwaji wa azimio la Seneti la kuunga mkono kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais.
Maseneta walipiga kura Oktoba 17, 2024 kumuondoa Naibu Rais Rigathi Gachagua baada ya Bunge la Taifa kupiga kura ya kumuondoa.
Mahakama Kuu pia imeamrisha kutishwa kwa mchakato wa kuteuliwa kwa mrithi wake hadi Oktoba 24, 2024, wakati kesi hiyo itakapofika mbele ya benchi la majaji watatu walioteuliwa na jaji mkuu Martha Koome.
"Kulingana na uzito ya masuala yaliyoibuka katika ombi lililoletwa nimedhihirisha kuwa suala hili linaibua masuala muhimu ya sheria na umma," Jaji Chacha Mwita wa Mahakama ya Kilimani alisema.
Ijumaa Oktoba 18, 2024, Bunge la Taifa lilipiga jumla ya kura 236 kumpitisha Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais wa Kenya, baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto.
Licha ya amri ya mahakama kusimamisha uteuzi wa Kindiki tayari uteuzi huo umeingia katika Gazeti la Serikali na kuonyesha kuwa amepitishwa na Bunge la Taifa kama Naibu Rais wa Kenya.